CCM kimeeleza kuwa, Dk. Jakaya Kikwete, mwenyekiti wa sasa wa chama hicho anatarajiwa kukabidhi uenyekiti wa chama hicho kwa Dk. John Magufuli tarehe 23 Julai mwaka huu.Taarifa iliyotolewa leo na Christopher Ole Sendeka, msemaji wa CCM inaeleza kuwa, mkutano maalum utafanyika katika ofisi ndogo za chama hicho Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam.
“Kamati Kuu imeridhishwa na maandalizi ya mkutano mkuu huo, Mkutano Mkuu maalum utatanguliwa na kikao cha sekretarieti, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa,” imeeleza taarifa hiyo.
Mei mwaka huu baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwepo kwa mgogoro ndani ya CCM kwamba, Dk. Kikwete kugoma kumkabidhi uenyekiti wa chama Dk. Magufuli, wiki iliyopita Mchungaji Gwajima aliibuka na kuishutumu CCM na mawakala wanaogomea Dk. Magufuli kukabidhiwa chama.
Mchungaji Gwajima aliishushia tuhuma CCM kwamba, lipo kundi la wanaCCM wanaozunguka sehemu mbalimbali nchini wakishawishi wanachama na wakimshawishi Dk. Kikwete ili aendelee na uenyekiti na kuleta hoja ya kutenganisha kofia ya Uenyekiti wa CCM na Urais wa nchi.
Kutokana na tuhuma hizo Ole Sendeka alisema, “napenda kuwafahamisha wana CCM, wapenzi wa CCM na wananchi kwa jumla kuwa, madai hayo ya Mchungaji Gwajima ni uongo mtupu na hayana hata chembe ya ukweli. Ni mambo ya uzushi na hadithi ya kufikirika.
“Watu hao hawapo kwani kama wangekuwepo habari hizo zingekwishajulikana chamani kupitia mfumo mahiri wa usalama na maadili wa ndani ya CCM.”
Muda mchache baada ya CCM kutoa taarifa hiyo, nyumba ya Mchungaji Gwajima iliyopo Mbezi Salasala ilizungumwa na polisi wakimsaka ambapo mkapa sasa inaripotiwa yupo nje ya nchi.
Tarehe 3 Mei mwaka huu Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa ya CCM ilikutana katika Ikulu ya Chamwino na kupitisha majina ya wagombea kwenye nafasi mbalimbali.
Kwenye mkutano huo Ole Sendeka alisema,“kimsingi kama ingekuwa ni kufuata Katiba ya CCM, Kikwete alitakiwa kukabidhi nafasi hiyo mwaka 2017 kwa malengo ya kutimiza kipindi cha miaka mitano lakini kutokana na utamaduni wetu, wameishakubaliana kukabidhiana majukumu hayo na sasa mandalizi yanafanyika.”
Post a Comment