Wakazi
wa Pemba wamelalamikia Jeshi la Polisi kuvamia maeneo yao na kupiga
mabomu ya machozi na kufanya doria usiku wa kuamikia juzi katika mitaa
na vijiji mbalimbali kisiwani humo na kuzua hofu miongoni mwao.
Maeneo
yaliyokabiliwa na hali hiyo ni pamoja na Mahuduthi, Kengeja, Mgagadu na
Kiwani, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ambako polisi wanadaiwa
kupiga mabomu ya machozi zaidi ya 100 na kutumia risasi za mpira
kuwatawanya watu.
“Ilikuwa
saa 1.30 usiku (wa kuamkia Jumamosi), gari za polisi zilifika kiamboni
(kijijini) kwetu zikipiga misere kwa kasi, sote tukawa na hofu, watu
walikimbia na kwenda kujificha, wengine waliumia na baadaye wakapiga
mabomu mfululizo, sijui waliondoka saa ngapi maana tulijifungia ndani,” alisimulia Zuberi Said (34), mkazi wa Kiwani.
Baadhi
ya wakazi wa vijiji hivyo walidai huenda hatua hiyo ya polisi ilitokana
na matukio ya kuhujumu mali za viongozi wa Shehia yanayoendelea.
Inadaiwa
kuwa watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Ijumaa waliteketeza miti na
mashamba yanayomilikiwa na Sabiha Mohamed Ali na Abdalla Makame Hamad,
ambao ni mashekha wa Shehia za Kendwa na Kiwani wilayani humo.
Ilidaiwa watu hao pia waliteketeza migomba na mikarafuu mali ya viongozi hao na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.
Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Hemed Suleiman Abdallah aliyefika kujionea uharibifu huo alisema: “Sijui sababu ni nini, ila huenda ni kutokana na siasa chafu zinazoendelea hapa.”
Alilitaka
Jeshi la Polisi na askari alioongozana nao katika ziara hiyo kufanya
uchunguzi haraka ili kuwabaini na kuwakamata watu waliohusika na vitendo
hivyo. “Wala msisubiri baada ya miezi 20 ndipo mkaanza kuchukua hatua,” alisema.
Kamanda
wa Polisi Wilaya ya Mkoani Pemba, Mohamed Salim aliyeambatana na Mkuu
wa Wilaya Abdalla, alikiri kuwapo kwa hujuma na kuwatuma askari katika
vijiji hivyo kufanya doria.
Post a Comment