Jumuiya ya Vijana CUF (JUVICUF) imeitaka Serikali kubeba mzigo wa kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa kuruhusu uingizwaji wa simu feki nchini.
Kauli ya jumuiya hiyo imekuja wakati imebaki mwezi mmoja kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuzima simu feki zote.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa JUVICUF, Mahamoud Mahinda Ally alisema Serikali ilishindwa kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha simu hizo haziingizwi nchini, hivyo inapaswa kuwajibika.
Ally alisema Serikali ilipaswa kuziba mianya hiyo tangu mwanzo na kwamba inachofanya sasa ni kukosa huruma kwa watu wake.
Alisema kitendo cha wananchi kuachwa wakinunua simu feki siku za nyuma bila ya kudhibiti uingizwaji wake nchini ni kutozingatia matakwa ya haki za binadamu.
“Kuruhusu simu feki ziingie nchini, kisha kuzizima ni mapambano ambayo Serikali inapambana dhidi ya wananchi wake,” alisema Ally.
Akizungumzia kuhusu hilo, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alisema mamlaka hiyo ilianza kutoa elimu kuhusu ya matumizi ya simu feki tangu mwaka 2010.
Alisema bado TCRA inaendelea na kampeni hiyo kwa wananchi juu ya madhara ya matumizi ya simu feki. Pia, alisema TCRA iliamua kufanya hivyo kutokana na majangili wanaotumia njia za panya kupitisha simu hizo na bila kulipa kodi.
Alisema wafanyabishara hao wasio waaminifu ndiyo wamechangia kuwapo kwa uingizaji wa simu feki nchini, licha ya Serikali kupiga marufuku.
Mungy alisema kutokana na wimbi la uingizwaji wa simu feki kuwa kubwa, waliamua kutumia teknolojia ya kuzima simu feki, ambayo itatumika kuanzia mwezi ujao ili kuwaepusha wananchi na bidhaa hizo kama zinazofanya nchi mbalimbali duniani.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA-CCC), Mary Msuya alisema simu feki kuingizwa nchini ni tatizo la wafanyabiashara wasio waaminifu.
Alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia njia za panya kuingiza bidhaa feki nchini. “Siyo simu tu hata bidhaa nyingine.”
Alisema ofisi yake ambayo ni washauri wa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini, imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu simu feki.
Alisema wananchi wamekuwa wishauriwa kuhakikisha kuwa wananunua simu katika maduka ya simu na wahakikishe wanapewa risiti ya dhamana ya muda wa matumizi ya bidhaa usiopungua miezi 12.
“Mteja asiponunua bidhaa feki hata mfanyabaishara atakosa soko,” alisema.Aliwataka wananchi kuzingatia mafunzo wanayopewa.
Post a Comment