Loading...

CHOZI LA KABWE KWA MAKONDA LIMETUA

 Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akiweka shada la maua katika jeneza la Marehemu Wilson Kabwe aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji
PAMOJA na kuelezwa kuwa umauti hauna adui, lakini kwa msiba huu wa Wilson Mbonea Kabwe umekuwa tofauti. Una maadui, tena maadui wasiofahamu maisha yake, utendaji na uadilifu wake katika kazi, anaandika Henerico Mayanja.
Hawa ni maadui waliojipambanua kuwa liwalo na liwe, lazima Kabwe aingie katika kitabu cha kumbukumbu za aibu, tena aibu ya tuhuma za wizi na ufisadi, licha ya kuwa na rekodi iliyotukuka katika maeneo mengi aliyofanya kazi.
Walioamua kuwa maadui wake, wanaongozwa na Paul Makonda, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, anayedaiwa kujiapiza kumng’oa Kabwe katika nafasi yake ya ukurugenzi wa jiji alilokuwa akiliongoza, akimwakilisha Rais John Pombe Magufuli.
Uadui wa Makonda kwa Kabwe unaelezwa na watu waliokuwa karibu na Kabwe na hata yeye mwenyewe kabla ya kukutwa na umauti Mei 20, mwaka huu.
Ieleweke kuwa utendaji uliotukuka wa Kabwe ndiyo umemfanya kuwa mkurugenzi wa majiji matatu kwa nyakati tofauti; Mbeya, Mwanza na baadaye Dar es Salaam, akiteuliwa na marais wawili; Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kuongoza na kusimamia kasma, fedha na utendaji wa majiji hayo kwa mafanikio makubwa.
Watu wanajuliza, endapo Kabwe angekuwa mwizi na fisadi ni namna gani angeweza kuaminiwa na marais wote hawa, tena akiwamo Mkapa ambaye umakini wake unasifika, siyo Tanzania tu, bali dunia yote.
Ukiacha sifa hizo za utendaji kutoka kwa marais hao, hata katika salamu za serikali wakati wa msiba wa Kabwe nyumbani kwake, Msasani, Dar es Salaam, George Simbachawene, waziri wa nchi, ofisi ya rais, tawala za mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi), alisema Tanzania imepoteza kiongozi mahiri na mwaminifu aliyeitumikia nafasi yake kwa umakini na weledi mkubwa kwa manufaa ya wananchi.
Kauli ya Simbachawene inaaminika na wengi waliokuwepo kwenye msiba huo kuwa inatoka kinywani kwake kwa dhati kabisa kwani alimfahamu Kabwe kwa muda mrefu na haina chembe ya unafiki uliozoeleka misibani.
Waziri huyo alisema- “kwa ngazi aliyokuwa amefikia Kabwe ni sawa na katibu mkuu wa wizara, leo hii ukiizungumzia Mwanza inayosifika kwa usafi na miundombinu, huwezi kuacha kumtaja Kabwe..
Alifanya mengi sana kwa ajili ya maendeleo ya Mwanza na maeneo mengine alikokuwa akifanya kazi za wananchi kwa niaba ya serikali, hakika serikali imepoteza mtumishi hodari na sisi tutaenzi mchango wake kwa kuendeleza mema aliyofanya Kabwe,” alisema Simbachawene.
Kauli hiyo ya Simbachawene na uteuzi wa kuaminiwa wa Mkapa na Kikwete ni ushahidi mwingine wa kutosha kuwa Kabwe hakuwa “mlaji,” alijitoa kufanya kazi za umma kwa uaminifu mkubwa na kupata fursa ya kutoa mchango wake katika kuendeleza majiji ya Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam.
Lakini pamoja na mchango mkubwa wa Kabwe, anajitokeza Makonda, kijana mdogo katika utendaji wa kazi za serikali na utumishi wa umma akiwaeleza Watanzania kuwa Kabwe ni mtuhumiwa wa ufisadi.
Bila aibu, mbele ya wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla wao, Makonda wakati wa ufunguzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere, linalounganisha Dar es Salaam na Kigamboni, alimchongea Kabwe na kumuonesha kuwa ni mtu asiyefaa.
Kwa staili ya Rais John Magufuli, bila kufanya utafiti alikubaliana na Makonda na kuamua kumsimamisha kazi Kabwe kwa tuhuma za kumdhalilisha, tena mbele ya umma.
Makonda alimchongea Kabwe Aprili 19 na baada ya siku 30, Kabwe mwenye miaka 60 alifariki dunia kwa ugonjwa ambao, pamoja na maelezo tofauti kuhusu chanzo cha kifo chake, upo uwezekano kuchangiwa na msongo wa mawazo kwa kudhalilishwa na kijana mdogo aliyeshindwa kuitambua vyema historia yake ya utendaji, hata kumwaminisha Rais Magufuli uongo.
Katika kutetea utu wake, Kabwe alisononeka mno kwa uamuzi wa Rais Magufuli na uchonganishi wa Makonda kwa kiongozi wa nchi.
Kabwe alisema; “mimi sihusiki na mikataba inayosemwa na Makonda, huu ni uongo mtupu, Makonda ametoa taarifa za uongo kwa Rais Magufuli akiwa na lengo la kunichafua na kunionesha mimi ni mtu wa hovyo ninayeendekeza ufisadi, hakika nimesikitika mno na kuumizwa.”
Aliongeza kueleza; “tuhuma zinazoelekezwa kwangu ni za uongo na zimelenga kunichafua mbele ya rais, nasisitiza tena hakuna mkataba wowote ambao ofisi yangu iliingia kwa nia ya kupoteza mapato ya serikali.”
Kabwe akaendelea kulalamika kwa uchungu; “hiki kinachodaiwa kupotea na Makonda kimepotea kutoka wapi?… huu ni upotoshaji wa wazi, hizo Sh. 3 bilioni zilichukuliwa na nani.”
Hadi mauti yanamkuta, Kabwe ndiye mkurugenzi pekee hadi sasa aliyewahi kuongoza majiji matatu Tanzania kwa nyakati tofauti na amekuwa na uzoefu wa miaka 19 katika uongozi wa serikali za mitaa.
Mbali na uzoefu huo, Kabwe ni mwanasheria, akiwa wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na pia mmoja ya wanabodi wa benki ya jamii Dar Es Salaam (DCB).
Wakati sifa zote hizo zikilazimishwa kufutwa na Makonda kwa kumchongea, na hatimaye kusimamishwa kazi na baadaye kukutwa na umauti, Makonda ameguswa, kusutwa na nafsi yake na kuukata mshipa wa aibu. Akajitokeza kwenda kuhani msiba.
Ni haki yake kwenda kuhani msiba wa Kabwe, lakini kwa jitihada zake binafsi kumchafua Kabwe kwa rais na mbele ya umma, imedhihirika kuwa mshipa wake wa aibu umekatika.
Kabwe amefariki dunia akilia. Akitoa chozi na sononeko la nafsi kwa namna alivyotendwa na kiongozi aliyeamua kumchongea tu kwa sababu anazojua yeye.
Sasa chozi la Wilson Mbonea Kabwe limekoma. Hatalia tena juu ya uso wa dunia, kwani limekatizwa na umauti. Alale salama.
Makala hii imeandikwa katika Gazeti la Mseto la tarehe 26 Mei mpaka tarehe 1 Juni mwaka huu katika ukurasa wa 5.

CHANZO: MWANAHALISIONLINE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top