Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), imevitoza faini vituo vya East
Africa Television na Entertaiment FM (E- FM) baada ya kukiuka kanuni za
utangazaji.
Akisoma nakala ya hukumu hiyo mbele ya waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA,
Joseph Mapunda alisema baada ya kupitia maelezo ya utetezi kutoka kwa
viongozi wa vituo hivyo, kamati hiyo imeamua kuitoza EATV faini ya Sh3
milioni na Sh4 milioni kwa E-Fm.
“Pamoja na adhabu hiyo tumetoa
onyo kali kwa kukiuka kanuni ya maudhui, lakini pia endapo kosa hili
litajirudia tunaahidi kutoa adhabu kali zaidi,” alisema.
Katika
maelezo ya awali ya hukumu hiyo, Mapunda alisema adhabu ya EATV
imetolewa baada ya kituo hicho kupitia kipindi chake cha muziki mnene
kurusha video ya wimbo wa Panya wa kundi la muziki la Bracket kutoka
nchini Nigeria uliomshirikisha msanii Techno.
“Baadhi ya mavazi
yaliyotumika katika wimbo huo hayaendani na maadili ya Kitanzania. Na
kwa upande wa E-FM wameadhibiwa baada ya kurusha kipindi cha Ubaoni
kilichotoa simulizi ya msichana mchawi aliyekiri kuua,”alisema Mapunda.
Baada
ya kupokea nakala ya hukumu hiyo, Mkurugenzi wa EATV, Regina Mengi
alisema hawana tatizo na adhabu hiyo na kwamba, atalifikisha suala hilo
kwa uongozi wa kampuni yao.
“Bado siwezi kujibu lolote, uamuzi wa kuikubali au kukata rufaa itategemea na uamuzi wa bodi,” alisema.
Mkurugenzi wa E-FM, Scolastica Mazula alisema ameridhishwa na hukumu iliyotolewa, hivyo haoni kama kuna sababu ya kukata rufaa.
Mamlaka
hiyo imevitaka vyombo vyote vya utangazaji nchini kuzingatia maadili na
taratibu za sheria zinapofanya kazi ili kuepuka kuleta athari katika
jamii.
Post a Comment