Spika wa Bunge, Job Ndugai, (pichani) amesema takribani asilimia 70 ya wabunge wa Bunge la 11 ni wapya hali inayolilazimu Bunge kuwapa mafunzo yatakayowawezesha kupambana na changamoto watakazokutana nazo wakati wa kufanya kazi za kamati.
Ndugai alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifunga mafunzo ya siku tano kwa wajumbe wote wa Kamati za Kudumu za Bunge yaliyoanza Januari 8 mwaka huu.
Alisema mafunzo hayo yanaibua changamoto ambazo kamati inakumbana nazo pamoja na kupata ufafanuzi wa masuala ya msingi kutoka katika Wizara, Idara,Taasisi na Wakala wa Serikali ambazo watakuwa wadau katika utekelezaji wa majukumu ya kamati.
“Natarajia mafunzo haya yatatumika kama nyenzo muhimu katika utendaji kazi wa siku hadi siku katika kamati zenu hasa ikizingatiwa kuwa idadi ya wabunge wengi kwenye bunge hili ni wapya,” alisema.
Alisema kuhusu mafunzo ya jinsi ya kufanya tathmini namna ya ufuatiliaji na utekelezaji wa bajeti, yatawapa uelewa wabunge wa masuala yanayohusu uchambuzi wa bajeti na mipango ya Serikali.
Ndugai alisema mpaka kumalizika kwa mafunzo hayo ya wabunge wa Bunge la 11 watakuwa na ujuzi wa msingi wa kuchambua masuala ya bajeti na mipango ya Serikali.
Alisema mipango pamoja na bajeti ya Serikali ina uhusiano wa moja kwa moja na wananchi katika majimbo wanakotoka wabunge na kwamba wanatarajia kuwa wananchi watanufaika na Bunge katika vikao vijavyo kutokana na weledi walioupata.
Katika mkutano huo wa mwisho wabunge walipata fursa ya kujifunza na kujadili kuhusu bajeti ya serikali na mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment