Loading...

Serikali Yatangaza Vita Dhidi ya Majambazi na Watu Wanaojihusisha na Mauaji

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni ametangaza vita dhidi ya majambazi na watu wanaojihusha na mauaji.

Alisema Serikali imelazimika kutangaza vita hivyo baada ya kutokea matukio 41 yaliyohusisha mauaji ya kinyama tangu Januari hadi mwezi uliopita.

“Serikali ipo kazini, sasa inatangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na ujambazi, watakaobainika hakika wataangamizwa hatuwezi kukubali watu wazidi kupoteza maisha pasipo na sababu za msingi,” alisema Masauni.

Waziri huyo alitembelea Msikiti wa Rahman Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, Mwanza na kusema matukio hayo yanapaswa kutokomezwa na kukemewa kwa nguvu zote.

 “Mauaji hayo yalikuwa ya kutisha hivyo ilikuwa ni lazima watuhumiwa wakamatwe, hata hao waliokimbia wanapaswa kutiwa mbaroni,” alisema.

Pia, alionya tabia ya baadhi ya polisi kujihusha na vitendo vya uhalifu na kupoteza imani na uaminifu kwa wananchi.

 Aliwataka polisi wanaofanya vitendo hivyo kuacha na badala yake wapambane na wahalifu.

Masauni alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa utulivu, hivyo haitakubali watu wachache kuvuruga amani iliyopo

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema vyombo vya usalama vipo imara kwani baadhi ya wahalifu wameuawa na wengine kukamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

Mjumbe wa baraza la masheikh Wilaya ya Nyamagana, Saidi Darwesh alisema tukio la mauaji ya msikitini limesababisha hofu kwa waumini, hususan kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kwani wengine hawaendi msikitini kuswali.

 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Utemini, Jukael Kiula alisema wakazi wa Kata ya Mkolani wamejitolea kujenga kituo cha polisi katika mtaa huo ili kudhibiti uhalifu unaotokea mara kwa mara.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top