Loading...

RIPOTI MAALUM: Machungu zaidi kwa familia siku 11 tangu mauaji Tanga

TAKRIBAN siku 11 tangu kutokea kwa mauaji ya kutisha yaliyohusisha watu wasiojulikana kuvamia baadhi ya nyumba na kuwachinja watu nane katika kitongoji cha Kibatini
Kata ya Mzizima Jijini Tanga, sasa waathirika wa tukio hilo wanakabiliwa na machungu mengine yanayohusiana na hali ngumu ya maisha katika eneo walilokimbilia kwa nia ya kujihakikishia usalama.
Baada ya tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Mei 31 na kuibua simanzi kubwa kutokana na namna lilivyofanyika, familia za ndugu wanane waliochinjwa na nyingine kadhaa za kitongoji cha Kibatini zilihama makazi yao na kwenda kuanza maisha mapya katika eneo la Kijiji cha Kona Z, umbali wa takriban kilomita 30 kutoka mahala walipokuwa wakiishia awali.
Wakati wakiyahama makazi yao, watu hao ambao baadhi walilazimika kuezua mabati ya nyumba zao na kubeba kila walichoweza kabla ya kuondoka ‘jumla’ Kibatini, walisema kilichowahamisha ni hofu ya usalama wao hasa baada ya kutopata taarifa za uhakika juu ya kukamatwa kwa watu waliotekeleza unyama huo na huku wakikumbuka kuwa wauaji waliahidi kurudi tena wakati wowote.
“Tulilazimika kuhama kwa sababu ya kusalimisha roho zetu… lakini sasa tunakumbana na hali ngumu ya maisha katika makazi mapya.
Kulala kwa tabu, na chakula pia shida. Cha kusikitisha, baadhi ya ahadi tulizopewa hazielekei kutekelezwa,” mmoja wa watu hao alimueleza mwandishi katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki.
Baada ya mauaji hayo ya kinyama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul alisema watu wasiojulikana, wakiwa na visu na mapanga, walivamia kaya tatu majira ya saa saba usiku na kuwaua watu wanane ambao ni pamoja na Issa Hussein (50), Mkola Hussein (40) na Hamis Issa (20) na Mikidadi (70).
Wengine ni Mahamud (35), Issa Ramadhani (25), Kadir (25) na Salum.
Taarifa za awali zilidai kuwa mauaji hayo yalitokana na kisasi baada ya awali kukamatwa kwa watoto wanane wa kigeni katika eneo la kijiji hicho na kisha polisi kuitwa na kuwakamata.
Ilidaiwa kuwa ndugu wa watoto hao wasiofahamika, na ambao walikuwa kwenye mapango ya Amboni yaliyo jirani na kijiji hicho, ndiyo waliotekeleza mauaji hayo ya kinyama dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Msako mkali dhidi ya wauaji hao bado unaendelea.
MACHUNGU MAPYA
Wakizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, baadhi ya watu waliohamia Kijiji cha Kona Z, walisema maisha yamekuwa magumu kwao na kinachowatia uchungu ni kutotekelezwa kwa baadhi ya ahadi na pia kuwapo kwa taarifa kuwa huenda siyo michango yote inayotolewa na wasamaria wema kwa ajili yao huwafikia.
Miongoni mwa viongozi waliowafariji wafiwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, Naibu Waziri wa Mambo ya ndani, Hamad Masauni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Watoto, Wazee na Walemavu, Ummy Mwalimu na pia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajab.
Katika eneo walilohamia sasa, watu hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za ukosefu wa makazi ya kudumu na familia zao, vyoo na pia huduma nyingine muhimu.
Hata hivyo, mwandishi ameshuhudia kuwa baadhi ya watu hao wangali wakihifadhiwa kwa ndugu na jamaa, ingawa vitu vya ndani vya wengi wao vimeishia kuhifadhiwa maeneo ya nje.
Akizungumzia misaada waliyoipata kutoka serikalini tangu kuhamia katika makazi yao mapya, Asha Hussein ambaye ni mke wa marehemu Hussein, alisema kuwa hadi sasa, kaya yake nyingine tatu zilizofiwa, wamepokea kila moja mifuko miwili ya tambi, maharage kilo 20, sukari kilo 20, unga wa sembe kilo 10 na majani ya chai kilo moja.
“Tunashukuru kwa msaada tuliopata… lakini ikibidi kuna haja ya kutusaidia zaidi kwa sababu hali yetu kwa sasa ni ngumu sana,” alisema Asha.
Aidha, mwandishi wa Nipashe amebaini kuwa kaya nyingine zilizokimbilia Kijiji cha Kona Z hazijapata misaada ya kiwango sawa na ile waliyopata wafiwa.
Msimamizi wa shughuli za mapokezi na msemaji wa wanajamii waliokimbia Kibatini, Mrisho Salim, alisema kuwa hadi sasa wamepokea rambirambi kwa awamu
Tatu, mara ya kwanza ilikuwa Sh. 100,000, mara ya pili Sh. 150,000 na ya tatu Sh. 100,000.
"Mpaka sasa tumepokea jumla ya Sh. 350,000 tu na fedha hizi hazina maelezo kuwa zimetoka kwa nani… hatujui kama ndani yake kuna rambirambi za viongozi zilizotokana na ahadi mbalimbali au la… ila kiwango hiki cha fedha hakilingana na idadi ya watu waliokimbia kule ili kunusuru maisha yao. Hali ni ngumu," alisema Mrisho, na kuomba wasaidiwe zaidi ili kuwapunguzia makali ya maisha wanayokabiliana nayo sasa katika eneo la ugenini.
Juma Issa Hussein, mtoto wa marehemu Hussein, alisema yeye anashangazwa na mabadiliko kuhusiana na ahadi ya kujengewa nyumba iliyotolewa na baadhi ya viongozi waliofika kuwafariji.
Alisema waliahidiwa kuwa zitajengwa nyumba nne kwa ajili ya familia nne zilizofiwa, lakini sasa zinazojengwa ni tatu badala ya nne.
"Kwakweli, nyumba nne bado zilikuwa hazikidhi haja kwa familia zilizofiwa… sasa zinajengwa nyumba tatu. Hatujui nani amebadilisha ahadi hiyo. Na jambo la pili ni kwamba nyumba tatu zinazojengwa ni za paa moja na siyo paa mbili kama tulivyoahidiwa.
Ila hatujui ni kitu gani kinaendelea maana ni msaada tu na sisi tunahitaji kusaidiwa kutokana na hali iliyopo, " alisema Juma.
Mzee Mlahangwa Maje, mmoja watu waliokimbia Kibatini na kuanza maisha mapya katika Kijiji cha Kona Z, alisema utoaji wa misaada unapaswa pia kuwafikiria wengine waliohamia hapo hata kama siyo miongoni mwa kaya nne zilizopoteza ndugu zao kwa vile wote ni waathirika wa kuwa wakimbizi wa muda ndani ya nchi yao kutokana na tishio la usalama
Alisema hadi sasa, kuna kaya takribani 30 zilizokimbia Kibatini na kwamba, kinachosikitisha ni kutotambuliwa kwa watu wengine wasiokuwa miongoni mwa kaya zilizofiwa.
"Waliohama Kibatini siyo wafiwa peke yao. Tumehama karibu wote kule kwa kuogopa kuuawa kwa sababu dalili zinaonyesha serikali imeshindwa kutuhakikishia usalama … sasa inakuwaje sisi hatufikiriwi kwa misaada?” alihoji na kuongeza:
“Wanaotambuliwa na viongozi na kufarijiwa ni wafiwa tu, hata nyumba zinazojengwa ni kwa ajili yao tu. Sisi wengine hatuna msaada na hata maeneo ya kukaa hatujapewa. Naomba na sisi watufikirie kwa sababu hatuwezi pia kuendelea kuishi kule. "
Hata hivyo, wakati Mzee Maje akiyasema hayo, Abdallah Shaaban ambaye ni Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM katika Kata ya Kiomoni, alisema serikali iko sahihi kuelekeza nguvu zaidi kwa wafiwa kutokana na machungu waliyoyapata ya kuondokewa na ndugu zao na kwamba, wengine walihama Kibatini kwa sababu ya matakwa yao binafsi na wala hawakuhamishwa na serikali ambayo mara kadhaa imewahakikishia kuwa usalama umeimarishwa na hawana sababu ya kuogopa.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top