Loading...

Polisi wachemka, CCM waandamana

 James Bwire, Meya wa Jiji la Mwanza
SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi nchini kupiga marufu maandamano na mikutano ya vyama vya siasa nchini, wafuasi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo wameandamana, anaandika Moses Mseti.
Maandamano ya CCM yamefanyika jijini Mwanza. Yameanzia katika Kata ya Mahina na kwenda kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Barabara ya Nyerere kisha kupokelewa na Idd Mkowa, Katibu wa CCM Wilaya.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi nchini lilipiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa kwa kile ilichodai kutokuwepo kwa hali nzuri ya usalama jambo ambalo limeibua mjadala kitaifa.
Hatua ya polisi kuzuia mikutano hiyo ilitokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  kutangaza kufanya mikutano ya hadhara ya kuishtaki serikali kwa wananchi kutokana na kuendesha nchi bila kufuata kanuni na sheria pamoja na kuzuia kuoneshwa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge.
Hata hivyo, baada ya Chadema kutangaza kufanya oparesheni hiyo iliopewa jina la ‘Okoa Demokrasia Nchini’ Polisi kupitia kwa Kamishna wa Mafunzo wa Polisi, ilizuia kufanyika kwa mikutano hiyo kwa kile ilichodai, hali ya usalama kuwa tete nchini.
Kutokana na zuio hilo, Chadema chini ya Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, kimekwenda mahakamani kuwashitaki Wakuu wa Polisi wa Wilaya za Geita na Kahama, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Polisi Makao Makuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Pamoja na kuwepo kwa katazo hilo, leo wafuasi wa chama tawala (CCM) wameandamana kwa madai kuwa James Bwire, Diwani wa Kata ya Mahina ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mwanza ananyanyaswa pia kutishiwa kuuawa na baadhi ya madiwani na watumishi wa jiji hilo ambao hawakutajwa majina.
Wanachama na wafuasi hao waliandamana wakiwa na mabango huku wakiimba nyimbo za chama hicho. Kwenye maandamano hayo polisi hawakuingilia kati.
Maandamano hayo yaliongozwa na Felician Balukali, Mwenyekiti wa Wazazi Kata ya Mahina na Teleza Chacha, Katibu wa CCM wa kata hiyo.
“Tunataka diwani wetu (James Bwire) awaachie umeya wao abaki kuwa diwani wa kushughulikia matatizo yetu, kwa nini anyanyaswe kama shida ni uongozi wao wabaki nao waendeleo nao,” amesema Chacha.
Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza akizungumza na waandishi wa wanahabari leo amedai kuwa, hana taarifa za tukio hilo na kwamba, polisi hawapo kwa ajili ya kukibeba chama chochote cha siasa licha ya kushindwa kuyazuia maandamano hayo.
Msangi ambaye pia ni Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) amesema, ” kwanza hilo tukio silifahamu ndio nasikia kutoka kwenu, nitalifuatilia kwa ukaribu na polisi hatupo kwa ajili ya kukilinda chama chochote kile cha siasa,” amesema.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top