MKE wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum (Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, inadaiwa amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo, akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.
Kamanda
wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia
waandishi wa habari jana kuwa mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa
mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.
Wakati
huo huo, Kamanda Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya
yaliyofanyika hivi karibuni Kigamboni na kusema polisi inaendelea
kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani aliyetoroka siku moja kabla ya
kifo cha mwanamke huyo.
Anayetuhumiwa kuua mumewe
Akizungumza
na waandishi wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu
yaliyojitokeza jijini Dar es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya
awali mke wa Kinyogori amekiri kuhusika.
Kwa
mujibu wa kamanda, mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake
kwa sababu za kipelelezi, aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo
baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke mwingine.
“Ni
jambo la kusikitisha kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa.
Tunawasihi wananchi kuepuka kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu
tu ya kuachwa wanawake wapo wengi na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa
na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai wa mtu,” alisisitiza Sirro.
Hata
hivyo, Sirro alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze
kuwataja watu wengine walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya
kuonekana kuwepo kwa wahusika wengine.
‘Hausigeli’ asakwa
Kuhusu
mauaji ya Anathe aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda
Sirro alisema wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo
ahojiwe kuhusu tukio hilo.
Aidha
alisema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku
polisi ikiwa imeandaa timu ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo
kufanikisha kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo.
Sirro
alisema msichana huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji
hivyo kupatikana kwake, kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka
kwake kulikuwa salama au kuna kitu kimejificha.
“Msichana
huyu tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi
juu ya kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani
tutafanikiwa kumpata na wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.
Mamia wajitokeza msibani
Vilio
na simanzi jana vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni
na Salasala walipokuwa wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30),
aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Mwili
ulichukuliwa jana asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na
kupelekwa nyumbani kwake Kibada, kwa ajili ya kuagwa na majirani zake
kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa mkoani Arusha leo.
Akizungumza
baada ya mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya
mtaa wa Nyakwale Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani
waliomba familia wapate fursa ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie
ana muda wa miezi sita.
“Baada
ya kuambiwa msiba upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe
fursa ya kuuaga mwili wa ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa
kweli msiba wake umetusikitisha sana” alisema.
Akizungumzia
tukio hilo alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4)
aliwataarifu majirani kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta
ameuawa.
Mwenyekiti
huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi na kuhimiza
wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa
vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama.
Post a Comment