MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imekwama kuendelea
kusikiliza ushahidi wa aliyekuwa mgombe ubunge wa Ukonga, Jerry Silaa
(CCM) baada ya kuwekewa pingamizi na upande wa walalamikiwa, anaandika Faki Sosi.
Pingamizi hilo la kukosoa ushahidi wa Silaa limetolewa na upande wa walalamikiwa kupitia Onesmo Kyauke, Wakili wa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), mbele ya Fatuma Msengi, Jaji katika mahakama hiyo.
Wakili Kyauke amedai kuwa, hatua ya kuweka pingamizi hilo inatokana
na shahidi (Silaa), kutoa ushahidi wake ambao upo nje ya kiapo.
Amesema kuwa, shahidi huyo amejibu swali wakati alipoulizwa na
wakili wake ambaye ni Dk. Masumbuko Lamwai kuhusu masanduku ya kura
kuchelewa kwenye baadhi ya vituo na kujibu nje ya kiapo chake, jambo
ambalo ni kinyume cha sheria.
Kutokana na sababu hiyo, Wakili Kyauke ameiomba mahakama kumzuia
shahidi huyo kutoendelea na ushahidi wake pamoja na kumzuia asijibu hoja
nje ya hati za kiapo.
Hata hivyo, Wakili Lamwai ameiomba mahakama kuliondoa pingamizi
hilo akidai kuwa kiapo chake kinaweza kujibiwa kwa maneno na sio
maandishi bila kuathiri kitu chochote.
Wakili Lamwai ametoa mfano wa rufaa ya kesi ya Zena ambayo
aliieleza mahakama kuwa, atajibu kwa hati ya maandishi lakini kwenye
maswali alijibu nje ya hati hiyo.
Kutokana na mvutano wa kisheria ambao uliibuka kutokana na
pingamizi hilo, Jaji Msengi ameahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili
ya kutoa uamuzi kuhusu ushahidi wa Silaa kuwa nje hati ya kiapo ama la.
Jana katika ushahidi wa kesi hiyo, Silaa alidai kuwa wafuasi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walimtishia kuchoma moto
nyumba yake wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Pia Silaa alidai Oktoba 27, mwaka jana katika kituo cha majumuisho
ya kupigia kura cha Pugu Sekondari idadi ya wapigakura wa Chadema
iliongozeka huku wakiwa wamesimama mita 20 kutokea usawa wa kituo cha
majumuisho.
Silaa ambaye aliwahi kuwa Meya wa Ilala alidai kuwa, wafuasi hao
walianza kuwatishia mawakala na msimamizi wa kituo jambo lililosababisha
Polisi washindwe kufanya kitu zaidi ya kuwaonya pamoja na kuzungumza
kihenyeji na mlalamikiwa wa pili.
“…kutokana na mazungumzo hayo, mjibu maombi wa pili na
wenzake walisema hawatopokea majibu ya kupiga kura na pia watachoma moto
nyumba yangu pamoja na kituo chenyewe,” alidai Silaa.
Post a Comment