Na Fatma Salum-MAELEZO, Dodoma.
Baraza
la Mitihani la Tanzania (NECTA) limejipanga kuanza kufunga bahasha
zenye karatasi za mitihani kwa kutumia mashine maalum ili kuondokana na
hatari ya kuvuja kwa mitihani hiyo na gharama za ufungaji wa mitihani
kwa kutumia mikono.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof.
Joyce Ndalichako wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara yake kwa mwaka 2016/2017, jana Bungeni Mjini Dodoma.
Prof.
Ndalichako alisema kuwa katika kuimarisha utendaji kazi wake NECTA
itanunua mashine mbili za kufunga mitihani (Auto Poly Wrapping and
Packing Machine) ili kuimarisha usalama wa mitihani kwa kupunguza watu
wanaoshiriki kwenye maandalizi ya mitihani hiyo.
“Katika
mwaka 2016/2017 Baraza litasimika mashine mbili za kufunga bahasha za
mitihani hivyo kuondoa hatari zinazoweza kujitokeza kwa kuwa idadi ya
watu wanaofanya kazi hiyo itapungua.” alisema Prof. Ndalichako.
Aidha,
Prof. Ndalichako aliongeza kuwa Baraza litaboresha mfumo wake wa
ukusanyaji na uchakati takwimu na kuweka Mfumo wa Kielektroniki wa
kumtambua mwanafunzi kwa namba maalum tangu anapoandikishwa shuleni hadi
atakapomaliza mzunguko wa masomo yake.
Alisema
kuwa mfumo huo wa utambuzi utaunganishwa nchi nzima ili kuwezesha
kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi kwenye shule yoyote atakayoenda
kusoma ndani ya nchi kwa kuwa namba hiyo atakayopewa na Baraza ataitumia
hata kwenye shule nyingine atakazohamia.
“Wizara
itaweka Mfumo wa Kielektroniki wa ukusanyaji taarifa za wanafunzi chini
ya Baraza la Mitihani ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa hizo
wakati wa mitihani na utaratibu huu utapunguza matumizi makubwa ya fedha
kupitia mfumo wa TSM9.” alisema Prof. Ndalichako.
Pia
alieleza kuwa katika kufanikisha Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),
mwaka wa fedha uliopita Mamlaka ya Elimu Tanzania imechapisha vitabu
558,720 vya jinsi ya kujibu mitihani ya Kidato cha Pili na Kidato cha
Nne ili kuwawezesha wanafunzi watahiniwa kujibu maswali vizuri katika
mitihani yao hatimaye kuongeza ufaulu.
Post a Comment