Loading...

Mahakama Kuu Kuanzishwa Katika Mkoani Mara

Mahakama ya Tanzania inakusudia kuanzisha Mahakama Kuu katika mkoa wa Mara ambapo ujenzi wa jengo la mahakama hiyo unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka huu.

Akizungumza leo mjini Musoma katika ziara yake ya ukaguzi wa shughuli za kimahakama katika kanda ya Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman alisema mkoa wa Mara unayo haki ya kuwa na Mahakama Kuu kwa kuwa nia ya Mahakama ni kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Alisema mahakama hiyo itajengwa kwa haraka na itamalizika katika kipindi cha mwaka moja kwa kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi huo tayari imeshatengwa ambapo nyingine imetokana na msaada waliopewa kutoka Benki ya Dunia.

Alisema kuanzishwa kwa mahakama hiyo katika Mkoa wa Mara kutawapa fursa wananchi wa Mara ya kupata huduma kwa karibu zaidi na pia itasaidia kupunguza kesi zilizoko mahakamani kwa haraka.

Awali akimkaribisha Jaji Mkuu ofisini kwake alipomtembelea, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo alimwomba Jaji Mkuu kuanzisha Mahakama Kuu katika mkoa wake kwa kuwa asilimia 55 ya kesi zote za mauaji katika Mahakama kuu kanda ya Mwanza zinatoka katika mkoa wa Mara hivyo mkoa huo unayo haki ya kuwa na Mahakama Kuu.

Pamoja na mkoa huo kuwa na kesi nyingi za mauaji, Mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa wa Mara pia unakabiliwa na kesi nyingi zinazohusu masuala ya ardhi kwa kuwa ni asilimia 38.3 tu ya eneo zima la mkoa huo ndiyo eneo linalotuwa kwa ajili ya makazi ya watu na shughuli za maendeleo
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Mara una wakazi zaidi ya milioni 1.3.

Alisema Mkoa wa Mara una eneo lenye kilometa za mraba 30,150 ambapo asilimia 36 ya eneo hilo ni maji wakati asilimia 25.7 ni eneo lenye mapori na hifadhi za Taifa ikiwemo mbugaya wanyama ya Serengeti.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa aliisifu Mahakama ya Tanzania kwa kufanya kazi yake kwa weledi ya kuzimaliza kesi zilizohusu mapigano ya koo zilizokuwepo katika siku za nyuma mkoani humo kwa kuwa zimesaidia maeneo ya mkoa huo kuwa salama hivi sasa na hayaonyeshi dalili za kujirudia. Aliongeza kuwa eneo la haki likitulia hata masuala ya utawala yakuwa rahisi.

Jaji mkuu Leo amehitimisaha ziara yake katika kanda ya Mwanza yenye mikoa ya Mara, Geita na Mwanza ambapo alikuwa akikagua shughuli mbalimbali za kimahakama katika kanda hiyo.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top