HABARI ya kuwepo kwa vijana wengi nchini hapa wanaojiunga na vikundi vya kigaidi ikiwemo Kundi la Dola ya Kiislam (IS) na Al-Shabaab imetikisha wengi, anaandika Faki Sosi.
Jana serikali imekiri taarifa ya kuwepo kwa idadi kubwa ya vijana wengi wanaokwenda kujiunga na vikundi hivi ambapo imeeleza kushtushwa kwake na taarifa hizo.
Kauli ya taifa kutambua uwepo wa vijana wanaojiunga na makundi hayo imetolewa jana bungeni mjini Dodoma na Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya Sh, trilioni 1.6 kwa mwaka wa fedha wa 2016/17.
Kwenye taarifa hiyo Dk. Mwinyi amesema, serikali inatambua kuwepo kwa harakati za vikundi hivyo na vijana wanaokwenda kujinga nao huku akisema, ili kuhakikisha nchi inakuwa salama, serikali inaendelea kupambana na makundi hayo katika maeneo yote ikiwemo mipakani.
Dk. Mwinyi amesema kwamba, katika maeneo yote duniani vitendo ama matukio ya kigaidi yamekuwa tishio kubwa na kwamba, kutokana na hali hiyo Tanzania nayo ipo macho ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari.
“Kuwapo kwa makundi ya Al-Shabaab, Al-Qaeda, Boko Haram na Islamic State, kunafanya tishio la ugaidi kusambaa duniani kote.
“Taarifa za kuwapo baadhi ya Watanzania wanaojiunga na makundi ya Al-Shabaab na ISIS tunazo, kunahatarisha usalama wa Tanzania, hasa ikizingatiwa kiujumla mwingiliano mkubwa uliopo kati ya wananchi wetu na watu wenye malengo tofauti.
“Hatari iliyopo ni uwezekano wa baadhi ya vijana waliojiunga na makundi ya kigaidi ya kimataifa kurejea nyumbani kwa lengo la kutekeleza vitendo vya kigaidi nchini mwetu.
“Tuna kila sababu ya kujizatiti na kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama,” amesema Dk. Mwinyi na kuongeza;
“Matukio yenye mwelekeo wa kigaidi, ni kama yaliyotokea katika mapango ya Amboni mkoani Tanga, Kitongoji cha Nyandeo wilayani Kilombero pale Morogoro na kukamatwa mabomu ya kutengenezwa kwa mkono katika maeneo mbalimbali yakiwamo Zanzibar.”
Dk. Mwinyi amewataka Watanzania kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya watu ama matukio yanayoashiria uvunjifu wa usalama.
Post a Comment