Wizara ya Elimu Sayansi Teknolojia na Ufundi imewasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2016/17 ya zaidi ya shilingi tirioni moja ambapo imesisitiza adhima ya serikali ya kutoa elimu bure huku wabunge wakihoji maamuzi ya tume ya vyuo vikuu kukifutia usajili chuo cha St Joseph.
Akiwasilisha bajeti hiyo yenye ongezeko la zaidi ya bilioni 300 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16, Prof Joyce Ndalichako ameyataja mazingira bora ya kufundishia, uimarishaji wa elimu, kuongeza idadi ya walimu ikiwa ni pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kufundisha hasa walimu wa sayansi kama moja ya vipaumbele vinavyokwenda kutekelezwa na bajeti hiyo kwa mwaka 2016/7.huku pia akigusia maamuzi ya TCU dhidi ya chuo cha St Joseph.
Bunge limeelezwa na kamati ya kudumu ya bunge kuwa elimu ya Tanzania imeshuka toka mwaka 2005, ambapo serikali imekuwa ikiridhika na wingi wa wanafunzi bila kujali ubora wa elimu, jambo lililosababishwa takwimu kuonyesha zaidi ya asilimia 45 ya wanafunzi hawajui kusoma na kuandika huku wakitaja pengo kati ya masikini na matajiri likizidi kuididimiza sekta ya elimu.
Kambi rasmi ya upinzani bungeni imeitaka serikali kuanza kutekeleza sera mpya ya elimu ya mwaka 2014, ambayo imejikita katika utoaji wa elimu ya msingi na sekondari bure, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa stahiki vya kufundishia, kuongeza ubora wa elimu na walimu ikiwa ni pamoja ukaguzi wa shule wa mara kwa mara.
Post a Comment