Loading...

BREAKING NEWS: MBUNGE wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo APATA PIGO ZITO AKIWA NDANI YA BUNGE NA KUPELEKEA KUBUBUJIKWA NA MACHOZI.

MBUNGE wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo alikaribia kutoa machozi bungeni jana wakati akihadithia mkasa wa maisha yake, aliposema wazazi wake wote wawili na mdogo wake waliliwa na mamba.
Mulugo, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi katika serikali iliyopita, pia aliitaka serikali imlipe fidia kwa vifo hivyo, na kutaarifu kuwa pamoja na ndugu hao, watu wengine 128 walikufa kwa njia hiyo katika Ziwa Rukwa.
Huzuni aliyoionyesha wakati akizungumza ilimfanya ashindwe kuendelea kuchangia kwa ufasaha hotuba ya makadirio ya Wizara ya Maliasili na Utalii, iliyowasilishwa juzi na Waziri Prof. Jumanne Maghembe.
Aidha, Mulugo alisema adui yake namba moja duniani ni mamba lakini hawezi kumpata kwa kuwa anaishi kwenye maji, hivyo adui yake namba mbili ni Prof. Maghembe na kumtaka kumpatia majibu lini atapewa fidia ya vifo hivyo.
Mulugo alisema uadui baina yake na Prof. Mghembe unaweza kupungua, hata hivyo, endapo waziri huyo
atatekeleza hatua zitakazopunguza uchungu wa waathiriwa.
“Nasema leo nisipopatiwa majibu ya uhakika nitashika shilingi ya Waziri," alisema Mulugo ambaye anakumbukwa kwa kudai Tanzania ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zimbabwe akiwa ziarani kama Naibu Waziri nje ya nchi.
"Mimi hapa ni yatima, nimepoteza baba, mama na mdogo wangu.
"Ninataka majibu leo… adui yangu namba mbili ni Magembe kwa sababu ndiye anayemtunza adui yangu namba moja.”
Alisema kuwa maelezo ya serikali kuwa inalipa fidia kwa waathirika walioliwa na mamba si ya kweli kwa sababu jimboni kwake kuna wananchi 128 waliofariki dunia kutokana na kuliwa na mamba.
Mulugu alibainisha kuwa Rukwa ni moja ya maziwa madogo Afrika, lililotengwa kwa ajili ya kufuga mamba na kwamba vifo vya watu hao vinasababishwa na serikali kwa kuvua mamba wachache wakati kasi ya kuzaliana inaongezeka kila siku.
Pia alisema hali hiyo imesababisha samaki kuisha ziwani humo kwa kuliwa na mamba.
Alisema wananchi wake wanaoishi vijiji vya Some, Manda, Udinde, Rukwa, Maleza na Mbangala wanategemea uvuvi kuendesha maisha yao, lakini pindi wanapofika katika ziwa hilo maisha yao wanayaweka reheni kwa sababu hawana uhakika kama watarudi salama nyumbani.
Alisema amewahi kuwasiliana na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, alipokuwa kwenye ziara jimboni humo na kumweleza kuwa serikali inapaswa kutenga fedha za kufanya utafiti wa kubaini kwa nini ziwa hilo halina samaki.
“Lakini hili halina mjadala samaki hawapo kwa sababu mamba ni wengi sana. Serikali inavuna mamba kidogo kwa mwaka kwa sababu vibali vinavyotolewa sharti vinataka wavunwe mamba 60 tu kwa mwaka.
"Watu wanauawa kila mwaka, waziri angalia hili suala jamani watu tunakufa.”
Aliongeza kuwa katika hospitali ya Mwambani Mkwajuni, kumejaa wagonjwa waliojeruhiwa na mamba, hivyo Waziri Maghembe anapaswa kupeleka watu katika ziwa hilo wakafanye utafiti kwa nini ziwa halina samaki na kwa nini mamba ni wengi hadi wanafikia hatua ya kudhuru watu kwa kiwango kikubwa.

    Post a Comment

    CodeNirvana
    Newer Posts Older Posts
    © Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
    Back To Top