MAAZIMIO ya Bunge kuhusu Richmond, Akaunti ya ‘Escrow’ pamoja na umiliki wa Kampuni ya IPTL yameibuka tena bungeni na kuipa serikali wakati mgumu, anaandika Faki Sosi.
Akiwasilisha Hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Nishati na Madini kuhusu Mapato na Matumizi katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, msemaji wa wizara hiyo John Mnyika ameibua upya hoja kuhusu utekelezwaji wa maazimio ya bunge. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba yake.
- UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU RICHMOND NA KUHUSU AKAUNTI YA ‘ESCROW’ YA TEGETA PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kurejea maamuzi/maazimio ambayo Bunge hili Tukufu lilikwisha yafanya kuhusiana na mikataba ambayo Serikali inaingia na makampuni mbalimbali hasa kwenye sekta ya nishati na madini.
Mheshimiwa Spika, Taarifa mbili za serikali kuhusu utekelezwaji wa maazimio haya ziliwasilishwa Bungeni tarehe 28 Agosti, 2008 na tarehe 11 Februari, 2009. Taarifa moja ilikabidhiwa na kujadiliwa na Kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge, yalifanyiwa kazi hadi mwezi Februari, 2009 na Maazimio 13 bado yalikuwa hayajakamilika.
Mheshimiwa Spika, Bunge liliazimia kwamba taarifa za utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo hata hivyo kuanzia mwaka 2011 mpaka mwaka huu wa 2016 kamati hiyo haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika hali ambayo inahitaji bunge kuingilia kati kuweza kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) na (3).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka Wizara ya Nishati na Madini na Serikali kwa ujumla kutoa majibu bungeni juu ya hatma ya maazimio 10 yaliyobaki: Azimio Namba 3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18 ili bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio husika yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka. Lakini hadi sasa tunaposoma hotuba hii maazimio hayo ya Bunge bado hayajatekelezwa na Bunge kupata mrejesho rasmi.
Mheshimiwa Spika, aidha Katika maazimio ya Bunge kuhusiana na fedha ufisadi uliofanyika katika akaunti ya “Tegeta escrow” na umiliki wa IPTL, maazimio yanayohusu sekta ya nishati na madini bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake, maazimio hayo yaliyotolewa na Bunge la Kumi, Mkutano wa Kumi na Saba katika kikao cha Ishirini kilichofanyika tarehe 29 Novemba, 2014 katika azimio namba 2,7 na 8.
Mheshimiwa Spika, Bunge katika azimio namba 2 liliazimia kwamba naomba kunukuu;
KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;
NA KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;
HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika kuona kwamba, mbali ya Serikali kushindwa kununua lakini bado inaendelea kulipia gharama za “capacity charges” na hivyo kuendelea kukiukwa kwa azimio ya Bunge. Hivyo basi tunamtaka Waziri alieleze Bunge ni kwa kiasi gani azimio hilo limetekezwa?
Mheshimiwa Spika, katika azimio namba 7 lililohusu kuwajibishwa kwa Mawaziri na watendaji wakuu wa wizara na Bodi ya Tanesco lilisema kwamba, nanukuu;
“KWA KUWA, vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;”
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais bila ya kujali nini Bunge lilikwisha azimia katika kikao ambacho na yeye alikuwa sehemu ya azimio hilo, lakini bado akamteua Mhe Prof. Muhongo kuendelea kuiongoza wizara hii. Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona jambo hili kama ni dharau sana kwa Bunge na ni fedheha binafsi kwake.
Mheshimiwa Spika, Bunge katika azimio namba 8 la taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya ‘escrow’ ya tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya Iptl iliazimiwa kwamba
“HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme”
Mheshimiwa Spika, Azimio hili linashabihiana na azimio namba 13 lililoazimiwa na Bunge wakati wa majadala wa taarifa ya kamati teule ya Richmond lililosema kwamba;
“……….. Kamati Teule inatoa wito kwa Serikali kuondokana na utaratibu huu usio na tija kwa kuzihusisha Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya mikataba hiyo. Aidha, Kamati Teule inatoa wito kwa Kamati zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba mikubwa na ya muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima. Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa kwa urasimu usio wa lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba iliyofichika”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imelazimika kunukuu maazimio hayo kutokana na ukweli kwamba Serikali imeshindwa kabisa kutekeleza maazimio ya Bunge, na badala yake mikataba hiyo inaendelea kutekelezwa kama ilivyoingiwa, mfano mzuri ni TANESCO kuendelea kuilipa IPTL fedha za capacity charge mpaka sasa. Jambo hili linazidi kuliondolea shirika hilo la umeme uwezo wa kuwahudumia wateja wake kwani haliwezi kuwekeza zaidi katika miundombinu za kusambaza umeme kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine wa mikataba yenye mashaka ni ule wa Mchuchuma na Liganga ambao NDC iliingia ubia na kampuni ya kichina ya HONGDA SICHUAN LTD na kuunda kampuni ya Ubia ya Tanzania China Internatinal Mineral Resource Ltd- TCIMRL katika kampuni hiyo ya ubia HONGDA SICHUAN LTD inamiliki asilimia 80 na NDC inamiliki asilimia 20.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wabia wanakuja mikono mitupu bila hela, sasa mbia mkubwa anatafuta mtaji kwa kutumia rasilimali za Kampuni ya ubia kama dhamana. Hizi rasilimali za Kampuni ya ubia ni zile zinazotakiwa kuchakatwa na kuuzwa, katika mazingira yoyote yale tukakubali vipi kuwa ubia wa njia hii unainufaisha nchi?
Mheshimiwa Spika, kama tunaweza kutumia rasilimali zetu kama dhamana ni kwanini tuingie ubia na tusitoe ajira kwa wataalamu waliobobea katika fani hizo na sisi tukawa na umiliki wa asilimia 100?
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema mikataba ya jinsi hii ndiyo itakayoliangamiza taifa letu, ni kwa nini wataalam wanaoingia mikataba ya namna hii wanatakiwa kuendelea kuwa maofisini?
Mheshimiwa Spika, licha ya ubabaishaji wa Kampuni hiyo ya Kichina bado ina uhakika kwamba mkopo wa kutumia rasilimali zetu ukipatikana ianze kuiuzia Tanesco umeme wa 600MW, hoja ya msingi je uhalali wa TANESCO kununua umeme wa Mchuchuma na Liganga utakuwa wapi?
Post a Comment