Mbali na fidia hiyo ya hasara ya jumla aliyoipata abiria huyo kutokana na safari hiyo kufutwa, pia Mahakama hiyo imeiamuru kampuni hiyo kumrejeshea abiria huyo nauli yake ya Sh43,000 alizokuwa ameshalipa na Sh339,000 alizozitumia kwa nauli baada ya kutafuta usafiri mbadala kutoka shirika jingine la ndege.
Uamuzi huo ulitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu Kisutu, Respicius Mwijage baada ya kuridhishwa na madai ya abiria huyo katika kesi aliyoifungua mahakamani hapo ya kampuni hiyo kuvunja mkataba.
Katika kesi hiyo ya madai namba 4 ya mwaka 2013, Mhozya ambaye pia ni wakili wa kujitegemea wa Mahakama Kuu, alikuwa akiiomba Mahakama iiamuru Fastjet imlipe Sh50,000,000, ikiwa ni hasara ya jumla aliyoipata pia imrejeshee fedha zake za nauli alizokuwa ameshalipa kwa mdaiwa pamoja na nauli aliyotumia kwa usafiri mbadala.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Mwijage alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote, hakuna shaka kwamba mdai na mdaiwa waliingia mkataba baada mdai kununua tiketi ambayo iliwasilishwa mahakamani kama kielelezo.
Alisema kwa mujibu wa mkataba huo, mdai alipaswa kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kurudi na kwamba kwa mujibu wa tiketi hiyo, mdaiwa alikuwa na wajibu wa kuwasiliana na mdai saa tatu kabla kuhusu kufutwa kwa safari.
Katika utetezi wake, mdaiwa kupitia kwa Ofisa Uhusiano na Ofisa Mtendaji, Lucy Mbogoro alidai kuwa baada ya kufuta safari walimtafuta mdai lakini simu yake ilikuwa haipatikani.
Hata hivyo, Hakimu Mwijage katika hukumu yake alisema hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa mahakamani kuonyesha kuwa baada ya kufuta safari walimtaarifu mdai kwa wakati kama inavyotakiwa kwenye tiketi.
“Mdaiwa hakujaribu hata kumleta shahidi kutoka kampuni ya huduma za simu za mikononi kuthibitisha madai yake kwamba siku hiyo mdai alipigiwa simu lakini hakupatikana,” alisema Hakimu Mwijage.
Licha ya mdai kueleza kuwa kufutwa kwa safari hiyo kulisababisha usumbufu katika kuhudhuria kesi za wateja wake na vikao muhimu, Mahakama ilisema fidia ya Sh50 milioni aliyoomba ni kubwa.
Post a Comment