Wakati Rais John Magufuli akiwa ameanza kazi kwa kuelekeza nguvu kuhakikisha huduma za afya zinaimarika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, huduma katika hospitali za rufaa na za mikoani hali ni mbaya zaidi, imefahamika.
Katika kitengo cha afya, Rais Magufuli alianza kwa kuhakikisha mashine
ya ST-Scan, MRI, vitanda, magodoro pamoja na mashuka vinapatikana katika
Hospitali ya Muhimbili.
Kadhalika, aliagiza kuhamishwa kwa Ofisi ya Wizara ya Afya iliyokuwapo
Muhimbili na kuligeuza eneo hilo kuwa wodi ya wazazi ambao walikuwa
wakilala wawili wawili na wengine chini.
Mbali na hilo, pia huduma ya maduka ya madaka chini ya Mamlaka ya
Chakula na Dawa (MSD), yalifunguliwa hospitalini hapo ikiwa ni mkakati
wa kuhakikisha wagonjwa wanapata dawa kwa urahisi na bei halali.
Hata hivyo, wakati Rais Magufuli akiendelea na juhudi hizo, uchunguzi wa
kina uliofanywa Nipashe katika hospitali kubwa za mikoa na zile za
rufaa, hali ni mbaya kutokana na kukosekana kwa huduma ya vipimo muhimu,
wauguzi, madaktari na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali.
Hospitali ya RUFAA Bombo
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, ambayo ndiyo
tegemezi na kimbilio la wakazi wa mkoa huo hasa kwa magonjwa ambayo
yameshindikana kupatiwa matibabu hospitali za wilaya ama vituo vya afya,
upatikanaji wa huduma si wa kuridhisha kutokana tatizo kubwa la ukosefu
wa watumishi na vipimo muhimu.
Kwa upande wa daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama, aliyepo ni mmoja
tu huku kukiwa na upungufu mkubwa wa wauguzi wakunga zaidi ya 40.
Batrice Rimoyi ni Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Bombo, ambaye anasema
kutokana na uhaba wa watumishi hasa kila muuguzi mkunga mmoja anaweza
kuwa na wastani wa kuhudumia akina mama zaidi ya 24 kwa akiwa zamu ya
saa nane.
Kwa mujibu wa Rimoyi ni kwamba kwa zamu moja takribani akina mama 48
wanapokelewa kwa ajili ya kujifungua ambao hudumiwa na wauguzi wawili tu
wakati wastani wa kawaida ni kila muuguzi ama mkunga mmoja kumhudumia
mama mmoja, jambo ambalo huwaweka katika wakati mgumu kwani baadhi
hujifungua kwa njia ya upasuaji.
Kwa upande wao akina mama wajawazito wakizungumzia hali halisi ya
upatikanaji wa huduma hospitalini hapo wanasema bado wanapata mashaka na
usalama wa maisha yao hasa kwa kuzingatia kuwa daktari bingwa wa
wanawake anayetegemewa ni hospitali nzima ni mmoja tu.
“Huko tunakotoka kuna vituo vya afya pia lakini tumepewa masharti kwamba
mimba ya kwanza lazima uje Bombo au kama wewe huwa unajifungua kwa njia
ya upasuaji unalazimika kuja huku sasa Daktari ni mmoja tu atuhudumia
wote kimsingi tatizo lipo pale pale kuna watakaopona na kuna watakaopata
madhara kutokana na hilo,” anasema Mariam Hamisi mmoja wa akina mama
anayepata huduma hospitalini hapo.
Kadhalika changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni uhaba wa wauguzi na
vitanda kutokana na wingi wa akina mama wanaopokelewa kupata huduma kwa
siku hivyo hulazimika kulala hata watatu kitanda kimoja.
“Kulala bado mtindo ni ule ule watatu kitanda kimoja na vitoto vyenu
labda wale waliopasuliwa siku ya kwanza utalala peke yako kesho yake
wanaletwa wengine hili ni tatizo kwa sababu hata maradhi ni rahisi
kuambukizwa,”alieleza Tumaini Hilali mmoja wa akina mama hao.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, akitoa taarifa ya
hali ya Hospitali hiyo kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa
katika ziara ya kikazi mkoani humo alisema hospitali hiyo inakabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi wa afya vitendea
kazi na uchakavu wa majengo hatua ambayo inakosesha ufanisi wa
kiutendaji na utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Mahiza alitaja miongoni mwa vifaa vinavyokosekana hospitalini hapo na
hivyo kuwakosesha wananchi kupata huduma bora za afya kwamba ni pamoja
na vifaa maalum vya uchunguzi ikiwamo CT-Scan, Echo na vitendanishi vya
maabara sambamba na uhaba wa wafanyakazi hasa wenye fani za ENT,
upasuaji wa mifupa, macho na mionzi.
Mkuu huyo wa mkoa.
Akizungumzia hali hiyo na changamoto za jumla za utoaji wa huduma za
afya kwa wajawazito Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita
anasema katika kukabiliana na hali hiyo wanaendelea kuboresha hospitali
za wilaya na vituo vya afya ili kuhakikisha wanaweza kupunguza
mlundikano wa wagonjwa katika hospitali hiyo ya rufaa.
HOSPITALI YA RUFAA Kitete
Katika Hospitali ya Rufaa Kitete mkoani Tabora, wajawazito walimpokea
mwandishi wetu kwa kilio cha kusikitishwa na huduma duni hospitalini
hapo hasa ukosefu wa dawa na vifaa tiba.
Akizungumza na Nipashe jana kwa niaba ya akina mama wenzake, Rukia Ally,
alisema katika wodi yao wanalazimika kulala wawili kwenye kitanda
kimoja pamoja na watoto wao baada ya kujifungua na wengine kulazimika
kujifungulia chini.
Rukia alisema kutokana na hali hiyo na msongamamo uliopo katika wodi
hiyo, kunasababisha kuambukizana magonjwa mbalimbali kwao na watoto.
''Sisi akina mama tunaolazwa hospitalini hapa inafikia wakati mwingine
unatandika kanga na kulala chini ili kujiepusha na mbanano katika
kitanda na mashuka kutoa harufu mbaya,” alisema Rukia.
Aidha, akina mama hao walimuomba Rais Magufuli majipu anayotumbua ya
pesa kwa mafisadi akumbuke kununua vifaa katika hospitali ya Rufaa
Kitete na kukarabati majengo.
Mganga Mkuu wa Mkoa katika Hospitali ya Kitete, Dk. Gunini Kamba,
alithibitisha kutokuwapo kwa madawa ya kutosha, vifaa tiba na kuwapo kwa
uchakavu wa majengo.
Alizungumzia wodi ya wazazi kuwa ni kweli kuna mrundikano wa akina mama,
lakini jengo hilo lina miaka mingi na idadi ya wazazi inaongezeka siku
hadi siku kutokana na kutokuwapo kwa hospitali za wilaya.
Katika wodi ya wazazi haiwezekani kuongeza vitanda kutokana na kutokuwa
na nafasi ya kutosha na mlundikano unatokana na zahanati nyingi zilizopo
mkoani kutokufanya kazi kwa saa 24, hivyo kusababisha wote kukimbilia
hospitali ya mkoa.
Aidha, Dk. Kamba alisema vifaa ambavyo vipo lakini vingine ‘vimekufa’ ni
x-ray ambazo zipo mbili lakini inayofanya kazi ni moja hali
inayosababisha mrundikano wa wagonjwa wa vipimo hivyo.
Alisema kifaa kingine cha magonjwa ya ubongo cha CT-Scan ni muhimu kuwapo katika hospitali hiyo lakini hakipo.
HOSPITALI YA RUFAA DODOMA
Kipimo cha cha X-Ray katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ni
moja ya changamoto kubwa kutokana na kuharibika tangu Januari mwaka huu
hali inayowalazimu wagonjwa kwenda Hospitali ya Mirembe.
Mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo, Aisha Ramadhani, aliliambia Nipashe
kuwa alimpeleka mwanawe ambaye amevunjika mguu lakini imewalazimu kwenda
Hospitali ya Mirembe kupiga X–Ray, umbali takribani kilomita tano.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Zainab Chaula, alikiri wagonjwa
wanaohitaji huduma ya X-ray kufuata nje ya hospitali hiyo huku akidai
imetokana na kipimo hicho kuharibika tangu Januari 13, mwaka huu.
Alisema taarifa za kuharibika mashine hiyo tayari zipo mamlaka husika na kifaa hicho kimeagizwa nje ya nchi.
“Inayotakiwa kuleta X-ray ni Wizara ya Afya na ni mpango wa serikali
kuzitengeneza zinapoharibika, na vifaa vyake havipatikani nchini hadi
nje ya nchi, tunasubiri wizara ituletee,”alisema Dk. Chaula huku
akiongeza kuwa pia hakuna vipimo vya MRI na CT-Scan.
Kadhalika Dk. Chaula alisema kuna upungufu wa watumishi 108 wa fani
mbalimbali ikiwa ni pamoja na madaktari bingwa saba, madaktari wasaidizi
tisa, maafisa wauguzi 15, wauguzi wa daraja la pili 22.
Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya
Katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya baadhi ya vipimo havipo
zikiwamo mashine za CT-Scan na MRI hali ambayo inawafanya wagonjwa
kukosa huduma inayohusu vipimo hivyo.
Akizungumza hali halisi, Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Thomas
Isdory, alisema kati ya vipimo hivyo vikubwa, hospitali hiyo inayo
mashine ya X-Ray pekee na kwambavingine viko katika mchakato.
Alisema kwa sasa wanafanya juhudi za kuhakikisha wanapata mashine ya
CT-Scan kwa mkopo kutoka katika Shirika la Bima la Taifa ambalo alidai
kuwa tayari wameshajaza fomu ya kuomba mkopo huo na kuipeleka wizarani
kwa ajili ya kuidhinishwa.
Kwa upande mwingine, Isdory alisema tatizo kubwa linaloikumba hospitali
hiyo ni upungufu wa madaktari bingwa pamoja na wafanya kazi wengine.
HOSPITALI YA RUFAA KCMC
Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi, inakabiliwa na changamoto lukuki
katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa wanaofikishwa katika
hospitali hiyo, ikiwamo kukosa mashine ya MRI.
Mbali na kukosa huduma hiyo, mashine nyingine za uchunguzi za CT-Scan na
mtambo wa upigaji picha za mionzi ya X-Ray zinafanya kazi kwa kiwango
kidogo kutokana na kuzeeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk. Gilliard Massenga
aliliambia Nipashe kwamba kipimo hicho cha MRI kinapatikana peke yake
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) na Hospitali nyingine za
Rufaa za KCMC na Bugando hazina mashine hiyo.
“Tunasubiri ahadi ya serikali, maana walitueleza watatuletea, lakini
sisi kimsingi hatuna mashine ya MRI, ila huwa tunawaandikia wagonjwa
waende Muhimbili. Na kuhusu CT-Scan na X Ray, mitambo hiyo inafanya kazi
taratibu mno.
Hiyo CT-Scan yenyewe ilinunuliwa kama mtumba mwaka 2006, kwa hiyo ina
umri mkubwa na maisha yake siyo marefu kwa sasa,”alisema Dk. Massenga.
Mbali na changomoto hiyo, KCMC kwa sasa ina vitanda 585 tu, ambavyo
kimsingi havitoshelezi mahitaji ya wagonjwa, ikilinganishwa na idadi ya
wagonjwa wanaofika kupata matibabu.
Kwa mujibu wa Dk. Massenga, hospitali hiyo yenye jumla ya wauguzi 242,
inakabiliwa na upungufu wa wauguzi 230 ili kukidhi mahitaji ya kuwa na
wauguzi 472.
Aidha, kwa upande wa waganga wanaohitajika kukabiliana na changamoto ya
wingi wa wagonjwa wanaofikishwa KCMC, walistahili kuwa na madaktari 164,
lakini waliopo kwa sasa ni 62.
HOSPITALI YA RUFAA BUGANDO
Mkurugezi Mkuu wa Hosptali hiyo, Kieni Mteta, aliliambia Nipashe
hospitali hiyo haijawai kuwa na mashine ya MRI huku ST-Scan tatu zipo
ambazo zimeisha kwa kuwa uwezo wa kufanya kazi ni miaka 10 na zilizopo
zina miaka 15, na kwamba katika bajeti yao ya 2016/2017 wameingiza
mpango wa manunuzi wa mashine hizo zikiwemo za X Ray ambazo nazo
zimeshachakaa.
Hospitali TEULE ya Tumbi
Hosptali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi ni kati ya hosptali
zinazotegemewa sana hapa nchini kutokana na umuhimu wake wa kuhudumia
wagonjwa mbalimbali hasa majeruhi wa ajali zinazotokea mara kwa mara
katika Barabara ya Morogoro.
Hata hivyo hosptali hiyo iliyojengwa na shirika la Elimu Kibaha mwaka
1967 anakabiliwa na matatizo lukuki ikiwa ni pamoja na tatizo la chumba
cha maiti.
Licha ya maiti nyingi zinazotokana na ajali kupelekwa hospitalini hapo,
kuna tatizo la majokufu kwani lililopo ni moja tu ambalo linafanya kazi
chumba kimoja chenye uwezo wa kubeba maiti nane.
Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Cyprian Mpemba, anasema licha ya
hosptali hiyo kupanda hadhi hadi kuteuliwa kuwa ya mkoa bado miundo
mbinu yake ni ya kizamani na ina matatizo ya vifaa tiba, madawa na
mashine mbalimbali za kumuhudumia majeruhi wa ajali.
Mganga Mkuu wa hosptali hiyo, Peter Dattani, kwa upande wake anasema
kuna upungufu wa wauguzi na madaktari na pia vyoo vilivyopo havikidhi
mahitaji ya sasa na kuwa hata chumba cha mapokezi hakitoshelezi mahitaji
ya wingi wa idadi ya watu 500 kwa siku wanaofika kutibiwa katika
hosptali hiyo.
Anasema upungufu wa mashuka nao ni changamoto nyingine inayoikabili hospitali hiyo.
Hospitali YA rufaa ya Mnazi mmoja Zanzibar
Kama ilivyo katika hospitali baadhi ya Tanzania Bara, matatizo hayo
yanalandana na yanayoikabili ya ile ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar.
Post a Comment