Loading...

WIZARA YA AFYA HAPATOSHI "DR. MWAKA" AKIONA CHA MOTO NA YUPO MATATANI SASA KWA KILICHOTOKEA KWENYE KLINIKI YAKE

 

Dk Mwaka 
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla ametoa siku saba kwa Baraza la Tiba Asilia kuchunguza huduma zinazotolewa kwenye kliniki ya Foreplan Herbal ya tiba mbadala inayomilikiwa na Dk Juma Mwaka.
Hatua hiyo ya Dk Kigwangalla imetokana na ziara ya kushtukiza aliyoifanya juzi katika kliniki hiyo iliyopo eneo la Bungoni wilayani Ilala Mkoa wa Dar es Salaam, lakini Dk Mwaka na baadhi ya wafanyakazi wa hawakuwapo wakati waziri huyo alipofika eneo hilo.
Hali hiyo ilimshtua Dk Kigwangalla, badala yake alishuhudia baadhi ya watoa huduma huku wagonjwa wakiwa wanasubiri kwenye vyumba ambavyo havikuwa na matabibu.
“Tunafahamu alikuwapo hapa na alikuwa anajua kuwa tunakuja, amepanda gari ameondoka dakika 10 zilizopita kabla sisi hatujafika hapa. Pia, walikuwapo matabibu, wafamasia, watu wa vipimo tukiwa hapa hapa, lakini wote mmewatorosha kupitia mlango wa nyuma. Kufanya hivyo si sahihi,” alisema Dk Kigwangalla na kuongeza:
“Nataka uanzishe uchunguzi kwa mujibu wa sheria kwa kutumia baraza lako la Tiba Asilia ili kubaini kama kituo kipo halali, tiba wanayotoa ni halali au si halali. “Kuna mambo yanayoendelea na wananchi wanalalamika kwenye jamii. Kwanza anajiita dokta wakati hana cheti cha kusomea udaktari halafu anatumia mambo yanayokwenda na taaluma ya udaktari wa kisasa.”
Mmoja wa matabibu wa kliniki hiyo, Teddy Mbuya ambaye baadaye alitajwa kuwa ni msaidizi wa Dk Mwaka, alikataa kuzungumza lolote kwa kuwa yeye si msemaji mkuu wa Foreplan.
Katika maagizo yake, Dk Kigwangalla amelitaka Baraza la Tiba Asilia kufanya uchunguzi ndani ya wiki moja, ili kubaini taaluma za watoa huduma kwenye kliniki hiyo, aina ya miti shamba inayotumika , dawa na watu wanaokwenda kutibiwa hapo ili Serikali ichukue hatua kwa mujibu wa sheria.
Pia, alimtaka Dk Mwaka kujisalimisha kwenye ofisi za wizara hiyo jana asubuhi.
Juhudi za kumpata Dk Mwaka kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa. Alipopigiwa simu, alipokea na kujitambulisha, lakini baada ya kujulishwa anazungumza na gazeti hili akadai kwamba yeye ni msaidizi wake na kuahidi kumjulisha mhusika kisha kukata simu.
Alipopigiwa tena alipokea mwanamke ambaye alijitambulisha kuwa ni msaidizi.
Dk Mwaka amejipatia umaarufu kama mmoja wa matabibu wa tiba asilia, hasa kutokana na vipindi vyake vya televisheni ambavyo huelezea matatizo mbalimbali ya binadamu na jinsi ya kuyatatua kwa kutumia tiba asili.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top