Loading...

SAKATA LINGINE TENA:..MAWAZIRI WA JK WATIMULIWA KWENYE NYUMBA ZA SERIKALI TENA WOTE KWANI MUDA WAO UMEISHA

Nyumba za Mawaziri zilizojengwa katika eneo la
Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakisubiri kufahamu sura zitakazoingia kwenye baraza jipya la mawaziri katika Serikali ya Rais John Magufuli, baadhi ya mawaziri wa awamu iliyopita ya Jakaya Kikwete hawajaziachia nyumba za Serikali walizokuwa wanaishi.
Kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma, mawaziri wanastahili kuishi kwenye nyumba za Serikali kuanzia pale uteuzi wao unapotangazwa ili kuanza kutekeleza majukumu yao wakiwa katika mazingira salama, wao na familia zao. Haki hiyo hukoma mara moja; pale wanapovuliwa wadhifa huo au baraza husika linapovunjwa baada ya kukamilisha muhula wake au sababu nyingine yoyote.
Maandalizi ya Rais Magufuli katika uteuzi yanakwenda sambamba na taasisi zinazohusika kutekeleza wajibu wao wa kuandaa makazi ya wateule wanaotarajiwa, lakini zinakwamishwa na mawaziri ambao hawajahama.
“Tumepata fedha za kutosha kukarabati nyumba zenye uhitaji huo kutoka wizarani. Nyumba 15 zipo katika utekelezaji. Kuna baadhi tunasubiri waliomo wahame ili tuweze kuendelea,” alisema Mhandisi Edwin Nnunduma, kaimu mkurugenzi wa ushauri wa Wakala wa Nyumba za Serikali Tanzania (TBA).
Nnunduma alisema kila kitu kipo tayari na mapokezi ya viongozi hao hautacheleweshwa kwa namna yoyote ile kwa kuwa nyumba zipo za kutosha kuwahifadhi ili walitumikie Taifa kwa viwango vinavyohitajika.
Takwimu zinaonyesha kuwa wakala huyo anasimamia jumla ya nyumba 93 na kati ya hizo 29 zilikuwa zinakaliwa na mawaziri wa Serikali iliyopita ya Rais Jakaya Kikwete ambao, kwa mujibu wa kanuni walistahili kuziachia mara tu baada ya Rais Magufuli kuapishwa, Novemba 5.
Kwa mujibu wa Nnunduma, ukarabati huo unahusisha nyumba 35 ambazo zinajumuisha 29 za mawaziri na sita wanazoishi baadhi ya makatibu wakuu wa wizara.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi zinaeleza kuwa wapo baadhi ya mawaziri ambao wamekaidi kuondoka kwenye nyumba hizo, licha ya kanuni na sheria kuwataka kufanya hivyo na agizo la Katibu Mkuu Kiongozi lilikwishatolewa likiwataka kurudisha magari na nyumba za Serikali.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mnunduma alisema, “Kuna waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi uliowataka wahame kwenye nyumba hizo ndani ya siku 30 baada ya kuapishwa kwa Rais mpya. Muda huo uliisha jana (juzi), naamini bado baadhi hawajahama mpaka sasa. Nilikuwa safarini hivyo sina uhakika ni nani na nani hawajafanya hivyo.”
Novemba 5, mara baada ya kuapishwa kwa Rais Magufuli, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, aliwaagiza mawaziri na manaibu waziri kurudisha magari ya Serikali ikiwa ni siku yao ya ukomo wa uongozi. Katika agizo hilo, alisema baada ya bendera ya Rais anayemaliza muda wake kuteremshwa na kabla ya ile ya Rais mpya kupandishwa, magari hayo yanatakiwa yabadilishwe namba kwa kuondoa herufi ya cheo na kuwekwa zile za Serikali.
Wakati urejeshaji wa magari ulifanywa mara moja, uhamaji kwenye nyumba za Serikali ulipewa muda wa siku hizo 30, ili kutoa fursa kwa familia husika kuandaa mazingira hayo ikiwa ni pamoja na kusafirisha mali husika za viongozi hao na walio nao.
Kukawia huko kwa baadhi ya mawaziri kunaelezwa kuwa huenda kukawa na sababu mbili; ama uhakika wa kurudi kwenye baraza jipya au kutokana na ukosefu wa mahali pa kuhamia baada ya utumishi kukamilika na muda wa kutafuta mahali pengine penye hadhi sawa na yao kuwa changamoto.
“Wapo baadhi ya mawaziri ambao walichaguliwa siku za mwisho ambao kabla ya hapo walikuwa wanaishi majimboni kwao. Mwezi mmoja uliotolewa unaweza usitoshe kwa wao kutafuta nyumba nyingine hapa mjini itakayowafaa kulingana na mahitaji yao,” kilisema chanzo ambacho hakikutaka kutajwa.
Uchunguzi wa gazeti hili katika mitaa Mikocheni, Masaki na Kijitonyama ziliko nyumba za mawaziri ulibaini baadhi zikifanyiwa ukarabati na baadhi ya walinzi waliohojiwa wakibainisha kuwa mawaziri wengi walishaondoka katika makazi hayo.
Hata hivyo, ofisa wa TBA anayeshughulikia makazi ya mawaziri Kanda ya Masaki, Juma Hamis alisema mawaziri waliokuwa wamebakia kwenye eneo lake ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Hawa Ghasia.
“Kwa taarifa nilizonazo, hawa mawaziri wanahama leo (jana) kwani tayari wameanza kuhamisha baadhi ya vitu vyao,” alisema Juma.
Hata hivyo, Makamba alipoulizwa alisema hajawahi kuishi kwenye nyumba ya Serikali tangu aanze kuwatumikia wananchi kwa nafasi tofauti alizowahi kuzitumikia.
Alisema, “Siku zote naishi kwenye nyumba yangu. Tangu nilipokuwa ikulu na hata nilipoondoka na kuwa waziri.”

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top