Baadhi ya Wafanyabiashara waliokwepa kodi wamejisalimisha na kulipa mabilioni ikiwa ni siku chache kufuatia tamko la rais John Magufuli kuwataka walipe kiasi chote cha kodi kabla ya siku saba.
Mamlaka ya Mapato nchini imeshakusanya takribani shilingi bilioni 8.6 tangu mwezi Disemba 2, ambazo zinajumuisha malipo ya kodi za makontena 349 yaliyopotea kwenye nyaraka za TRA bandarini.
Taarifa ya TRA kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa kiasi hicho kilikusanywa kutoka kwa makampuni ya Sadid Salum Bakhresa (bilioni 2), Tifo Global Trading Company Ltd (milioni 310), ips Roofing Company Ltd (milioni 80), Red Building Company Ltd (milioni 100), Zing Enterprises (milioni 325.6) na Sapato N Kyando (Milioni 50.5).
“TRA inaendelea kuwasisitiza wafanyabiashara ambao makontena yao na mizigo yao yamepita katika bandari ya Dar es Salaam au mpaka wowote bila kulipa kodi, kuhakikisha wanalipa madeni ya kodi zao ndani ya siku zilizobaki tangu kutolewa agizo la ukomo,” ilieleza taarifa ya TRA kwa vyombo vya habari.
Ilieleza kuwa endapo ukomo wa siku hizo utafika, TRA itachukua hatua za kisheria kuhakikisha madeni yote ya kodi yanalipwa.
Rais John Magufuli aliwataka wafanyabiashara wote waliokwepa kodi kuhakikisha wanalipa kodi zao kabla ya siku saba (kuanzia Disemba 4 mwaka huu).
Post a Comment