Loading...

Wabunge walizwa, Zitto akoleza

 Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini
ZITTO Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo amekoleza moto wa wabunge kukatwa kodi katika fedha za kiinua mgogo, anaandika Dany Tibason.
Wakati hayo yakifanyika, Serikali ya Rais John Magufuli imewang’oa wabunge wa viti maalumu kushiriki kwenye Kamati za Fedha na Mipango za Halmashauri.
Jumatano wiki hii serikali ilisoma bajeti yake ya Sh. 29. 52 kwa Mwaka wa Fedha 2016/17, sehemu ya bajeti hiyo ilionekana kukera wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mheshimiwa spika, natangaza kufuta msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utoaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi,” alisema Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango.
Kutokana na mpango huo wa serikali kutoza kodi katika kiinua mgongo cha wabunge na kuzua zogo kwa wabunge wa CCM, Zitto amesema, ni vema serikali ikafanya hivyo ili kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi kwa ajili ya kuendesha nchi.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini amekwenda mbali zaidi na kusema kwamba, Bunge halipaswi kuishia kwenye kodi hiyo pekee kwa kuwa, kuna kodi nyingi za wabunge ambazo hazijaguswa.
Kauli hio ni mwendelezo wa msimamo wake wa kupinga wabunge kulipwa posho za vikao vya bunge. Katika kampeni yake kwenye Bunge la 10, Zitto hakufanikiwa kuondoa posho hiyo.
Zitto ametoa msimamo wake kuhusu kukata kodi wabunge wakati akitoa maoni yake kwenye uchambuzi wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu za KPMG juzi.
Hata hivyo Zitto amesema kwamba, pamoja na serikali kuanzisha kiinua mgongo hicho lakini hakuna sheria yoyote inayoruhusu kitu hicho kufanyika na hivyo kuonesha kushangazwa na hatua hiyo.
Hatua ya Zitto bila shaka itakoleza mjadala wa posho ambao tayari CCM wameonesha kukerwa na hatua ya serikali kuanza kutoza kodi hiyo.
Wakati Waziri Mpango akiwasilisha bajeti hiyo na kufikia kipengele kinachoelekeza kuwa, kodi hiyo itaanza kukatwa, wabunge wa CCM ambao ndio pekee waliokuwa bungeni, walianza kuguna hatua mbayo ilimlazimu Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge kuingilia kati na kutuwatuliza.
Wakati hayo yakiendelea, serikali imeendelea kuwakomba posho wabunge baada ya Seleman Jafo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kueleza kuwa, wabunge wa viti maalum ni marufuku kushiriki kwenye Kamati za Fedha na Mipango za Halmashauri.
Jafo amesema, kwa mujibu wa sheria za Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji, wabunge hao hawaruhusu kushiriki kwenye kamati hizo.
Na kwamba, ili wabunge hao waweze kushiriki kwenye kamati hizo, inahitajika kubadili sheria kwanza ili pendekezo hilo liweze kutekelezeka.
Jafo ametoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la Martha Umbula, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) na kwamba, Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Halmashauri wametajwa katika kifungu cha 75(6) cha sheria sura 287 Mamlaka za Wilaya na
kifungu cha 47(4) cha Sheria Sura 288 Mamlaka za Miji.
“Kwa mujibu wa sheria hizo mbili wajumbe wa Kamati hawatazidi theluthi ya Madiwani wote isipokuwa Kamati ya Fedha na Mipango ambayo wajumbe wake ni wale wanaoingia kwa nyadhifa zao,” amesema Jafo.
Amesema, upatikanaji wa wajumbe wa kamati hiyo umefafanuliwa katika Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa kila Halmashauri.
Ameaja wajumbe wake kuwa ni Mwenyekiti au Meya wa Halmashauri, Makamu au Naibu Meya, Mbunge au wabunge wa majimbo, wenyeviti wa kamati za kudumu na wajumbe wasiozidi wawili.
Amesema, wajumbe wa Kamati ya Fedha wataendelea kuwa hao waliotajwa katika Sheria na Kanuni za Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi hapo
sheria itakapofanyiwa marekebisho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top