Loading...

MUHIMU: FAHAMU NAMNA YA KUJITAMBUA JINSI ULIVYO


Siku moja niliona kwenye televisheni mahojiano kati ya mtangazaji na kiongozi mmoja mashuhuri katika nchi fulani. Wakati huo katika nchi hiyo Uchaguzi Mkuu ulikuwa umekaribia.
Hivyo, mtangazaji alimuuliza yule kiongozi kama alikuwa akitarajia kugombea urais wa nchi hiyo kwa kuwa aliyekuwa madarakani alikuwa anamaliza kipindi chake.
Yule kiongozi alimwambia mtangazaji kuwa yeye ana tabia ya kujitazama kwenye kioo kila siku asubuhi kabla hajatoka nje. Aliendelea kusema kuwa siku zote anapojitazama kwenye kioo hajawahi hata mara moja kujiona kuwa yeye ana wajihi unaofaa kwa kuwa rais.
Yule mtangazaji alipomwuuliza yule kiongozi anawezaje kwa kujitazama tu kwenye kioo kutambua kama anafaa au hafai kuwa rais, alielezea habari nyingine hadi muda wa kipindi ukaisha bila kujibu swali hilo.
Je wewe unajitambua jinsi ulivyo? Je unapochukua kioo ukajitazama unaweza kujitambua wewe ni mtu wa namna gani au unaweza tu kutambua jinsi sura yako ilivyo. Nasita kusema kama kioo kitakaonyesha jinsi sura yako inavyoonekana kwa kuwa watu wanaweza kutofautiana kwa jinsi wanavyoiona sura yako. Labda nikuulize swali jingine je kwa kujitazama kwenye kioo unaweza kupata viashiria vya mabadiliko unayostahili kuyafanya ili uwe mtu tofauti na ulivyo sasa. Sijui jibu lako litakavyokuwa kuhusu jinsi unavyoweza kukitumia kioo kikusaidie kujitambua, lakini mimi nimejaribu mara nyingi kujitazama, lakini hakikuweza kunisaidia kujitambua jinsi nilivyo.
Kitu kimoja muhimu zaidi kuliko vyote katika maisha ya binadamu ni kuwa na tabia nzuri na inayowapendeza na kuwavutia watu. Tunapokuwa watoto wazazi, walimu na jamii hujitahidi kutufunza mienendo mizuri na tabia njema.
Hata hivyo, kadri tunavyokua kuna baadhi ya tabia huziacha na pengine kuongeza nyingine. Bila kujali mchanganyiko wa tabia tunazokuwa nazo tunapokuwa watu wazima, wajibu wa kuhakikisha tunakuwa na tabia na mwenendo unaofaa katika jamii unakuwa mikononi mwetu.
Je tunaweza kushika hatamu za mienendo yetu. Hatuna budi kujitambua jinsi tulivyo na namna tunavyoonekana kwa watu wengine. Aidha, tunalazimika kubaini kama kuna mambo dhaifu tunayostahili kuyabadili ili tuwe na tabia bora.
Hata hivyo, ni kitu gani kinaweza kutusaidia kujichunguza sisi wenyewe? Tunaweza kujichunguza kwa kutumia hisia binafsi. Mtu anaweza kutenda jambo fulani njiani wakati akielekea nyumbani. Anapofika anaweza kukaa peke yake akawaza na kusema na nafsi yake yeye mwenyewe “Jambo lile nililofanya halikuwa zuri. Sitarudia tena kufanya hivyo.” Kile kinachomfanya ajisahihishe yeye mwenyewe ndicho kinachoitwa hisia binafsi. Hii ndiyo inayomsaidia mtu kujitambua jinsi alivyo na hata kumfanya aweze kupeleka mawazo yake mbele na kubaini inafaa aweje baadaye. Kwa kuzingatia kanuni hii inambidi kila mtu kujenga au kuimarisha hisia binafsi katika akili yake ili aishi akijitambua wakati wote na kujirekebisha kila inapobidi. Wala tusiwe na mawazo yasiyo sahihi ambayo baadhi ya watu huwa nayo wakasema: “Nimechelewa muda umepita na sasa hakuna ninachoweza kufanya ili kubadili tabia yangu.”
Mwanafalsafa mmoja alisema maisha ya mtu ni kama kitabu. Kila siku anayoishi anaandika ukurasa mpya. Hawezi kubadili kurasa zilizopita, lakini anaweza kuhakikisha kila ukurasa mpya unaofuata anaufanya kuwa mzuri zaidi kuliko ule uliopita. Hivyo ndivyo inayobidi tuishi.
Tunawezaje kujenga au kuimarisha hisia binafsi zetu?
Tunajenga hisia binafsi kadri tunavyoishi na kuutambua ulimwengu kwa kutumia milango ya fahamu. Kwa mfano; kijana anapofua au kutupa nguo zake ovyo ovyo na akawasikia wazazi wake wakigomba na kusema: “Wewe ni mtoto mbaya hutakiwi kuzifanya nguo zako hivyo.” Wakati anapozifua, akazipiga pasi na kuzipanga sandukuni na kisha akawasikia wazazi wake wakisema: “Wewe ni mtoto mzuri kwa kuwa unatunza nguo zako.” Iwapo hali itaendelea vivyo hivyo na kijana akawa anasikiliza maneno hayo siku baada ya siku, mwezi hadi mwezi, na mwaka mmoja hadi mwingine hupata funzo kuu katika maisha. Nalo ni hili, yeye ni kijana mbaya anapofanya mambo mabaya na kujifanya asipendwe, lakini anapofanya mambo mazuri anakuwa kijana mzuri na anajifanya apendwe.
Pia kama kijana huyo njiani huwa anawapita watu waliokaa kwenye kibaraza cha nyumba yao bila kusema chochote hakuna lolote litakatokea. Lakini siku moja akiamua kuwasalimu watamwitikia kwa furaha. Baada ya hapo siku nyingine akipita hata kama atakaa kimya watu hao watamchangamkia na kumsalimu. Hapana shaka hilo litakuwa somo kwake kwamba wameunda mawasiliano ambayo yamewajengea mazingira rafiki.
Hivyo, ndivyo hisia binafsi inavyojengeka kutokana na mchanganyiko wa taarifa na mwitikio kutoka kwa watu wengine. Aidha, tunabaini kuwa hisia binafsi hujengeka kutokana na jinsi tunavyojifunza, kupata uzoefu na mrejesho tunayopata kutokana na watu wengine.
Tunawezaje kuamua jinsi tunavyotaka tuwe baadaye
Baada ya kujua jinsi tunavyo baki na changamoto ya kubadilika ili tuwe watu bora zaidi kuliko tulivyo. Kwa kutumia hisia binafsi tunaweza kutumia mbinu ya kuigiza watu wengine. Chagua mtu anayekuvutia sana katika maisha yako. Anaweza kuwa angali hai au amefariki. Orodhesha mambo yanayokufurahisha kutokana na jinsi ilivyo. Mtu mmoja alipoulizwa mtu anayemvutia sana katika maisha yake alimtaja Nelso Mandela. Alipoulizwa sababu ya kuvutiwa naye alisema kwa sababu alikuwa mtu aliyeheshimiwa na kupendwa kutokana na upendo wa dhati aliokuwa nao kwa watu na taifa lake. Alikuwa tayari kuteseka ili wengine wapate heshima, haki na uhuru.
Tunapozichunguza sifa za Mandela alizozitaja mtu huyo tunapata picha kuwa ndizo tabia anazozipenda katika maisha yake. Huenda baadhi ya hizo yeye anazo na kama hanazo angependelea awe nazo. Huu ndio mchakato wa mawazo ambao unaweza kumfanya mtu kuwa na hisia za jinsi ambavyo angependa awe.
Kutokana na niliyoyandika katika makala hii hatuna budi kufanya kila juhudi ili tuweze kujitambua jinsi tulivyo. Tunapojitambua tulivyo tunapata fursa ya kuboresha hali zetu ili tuwe watu bora zaidi.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top