BAJETI ya serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 iliyosomwa jana, imekera wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Faki Sosi.
Wabunge hao wameonesha kukerwa na bajeti hiyo pale Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango alipogusa maslahi yao ya kiinua mgongo.“Mheshimiwa spika, natangaza msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utoaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi,” amesema Dk. Mpango katika hotuba yake.
Wabunge wa CCM ambao ndio waliokuwa wamebaki bungeni kutokana na wale wa upinzani kutoka nje, walionekana kutoridhia mpango huo jambo ambalo lilizidisha minong’ono na kusababisha Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge kuingilia kati na kuwatuliza.
Kabla ya Dk. Mpango kufikia kipengele cha kuondoa msamaha wa kodi kwenye kiinua mgongo hicho, wabunge walifanya kazi ya kugonga meza kila ambapo msoma bajeti alipoweka nukta katika usomaji wake.
Hata hivyo, Dk. Mpango amesema, lengo la serikali ni kufunga mkanda kwenye bajeti hiyo ili kuhakikisha inafikia malengo yake ya kupata fedha kukamilisha bajeti yake ya jumla ya Sh. 29.52 trilioni kwa mwaka huu wa fedha 2016/17.
Bajeti hii iliyosomwa na Dk. Mpango, ndio ya kwanza katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.
Pia, ndio bajeti ya kwanza tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 iliyosomwa bila kuwepo kwa wabunge wa vyama vya upinzani ambao walitoka ikiwa ni mwendelezo wa kugomea vikao vyote vya Bunge vinavyoendeshwa na Dk. Tulia kwa madai ya kupendelea CCM.
Dk. Mpango akisoma bajeti hiyo kuanzia jana saa 10 jioni alisema kuwa, bajeti hiyo imedhamiria kutekeleza ahadi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kama zilivyoainishwa katika Ilani ya CCM wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana.
Lakini pia amesema inakwenda sambamba na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Dk. Mpango amesema kuwa, serikali imekusudia kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi wa chini ikiwa ni pamoja na kudhibiti mianya ya rushwa sambamba na ufujaji wa fedha za umma nchini.
Katika bajeti hiyo, kodi mbalimbali zimeongezwa ikiwa ni pamoja na kodi ya usajili wa magari kutoka Sh. 150,000 na kufikia Sh. 250,000 na bodaboda kutoka Sh. 45,000 hadi Sh. 90,000.
Kodi ya usajili binafsi wa magari imeongezeka kutoka Sh.5 milioni kwa miaka mitatu hadi Sh. 10 milioni kwa mwaka, pia kodi ya vileo imeongezwa ambapo bei rasmi itaanza kutumika Julai mosi mwaka huu.
Pia serikali imepandisha kodi kwenye uingizaji wa nguo na viatu vya mitumba kutoka nje ya nchi na kwamba, lengo ni kulinda bidhaa za aina hiyo zinazozalishwa na viwanda vya ndani ya nchi.
Akizungumzia udhibiti wa fedha za serikali Dk. Mpango amesema kuwa, kuanzia Julai mosi ni marufuku kwa wizara, taasisi, wakala wa serikali, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kufanya biashara na wazabuni na wafanyabiashara wengine ambao hawatotumia mashine za kulipia kodi kwa njia ya kielekroniki (EFDs).
Na kwamba, mapato ambayo yatalipwa bila kuwepo kwa stakabadhi za mashine hizo ni lazima ziambatanishwe na ushahidi kwamba, mfanyabiashara ametangazwa rasmi na Kamishna wa Mapato kutotumia mashine za EFDs.
Katika hatua nyingine serikali kupitia Dk. Mpango imetangaza kuwa, tayari imetenga jumla ya Sh. 2.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Mafisadi.
Uanzishwaji wa mahakama hii ulikuwa sehemu ya ahadi ya Rais Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.
Pamoja na hivyo, serikali imetenga Sh. 72.3 kwa ajili ya shughuli za ndani ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) huku jumla ya Sh. 44.7 bilioni zikitengwa kwa ajili ya shughuli za Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Bejeti hiyo ni ongezeko la asilimia 7.04 sawa na asilimia 31 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16 ya Sh. 22.49.
Post a Comment