Watanzania walio wengi (79%) hawakubaliani na maamuzi ya serikali ya kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia runinga na redio.
Karibu wananchi wote (92%) wanaamini kuwa ni muhimu vikao hivyo virushwe moja kwa moja.
Takwimu hizi zimetolewa na Twaweza kupitia muhtasari wa matokeo ya utafiti wake: #BungeLive.
Muhtasari huo unahusisha takwimu zilizokusanywa na Sautiza Wananchi, Utafiti wa kwanza barani Afrika unaotumia simu za mkononi na wenye uwakilishi wa kitaifa.
Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,815 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 29 Machi na tarehe 12 Aprili 2016.
Miongoni mwa watanzania waliokua wakitazama na kusikiliza vipindi vya Bunge asilimia 42 walikuwa
wakiangalia vikao vya Bunge vilivyokuwa vikirushwa moja kwa moja kupitia runinga na asilimia 60
walikuwa wakisikiliza vikao hivyo kupitia redio. Kati ya hawa, asilimia 59 waliangalia vipindi vya Bunge kupitia runinga miezi miwili kabla ya utafiti huu kufanyika, na asilimia 57% walisikiliza vipindi vya Bunge kupitia redio.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa wananchi walikuwa wafuatiliaji wazuri wa vikao vya Bunge vilivyokuwa
vikirushwa moja kwa moja. Sababu zao za msingi ni kama zifuatavyo:
• Asilimia 46 ya wananchi wanataka kuwafuatilia wabunge wao ili kuona kama wanawawakilisha
ipasavyo.
• Asilimia 44 ya wananchi wanasema ni haki yao kufahamu kile kinachoendelea bungeni
• Asilimia 29 ya wananchi wanaamini zaidi matangazo ya moja kwa moja kwa sababu wanawaona na
kuwasikia wabunge kwa macho na masikio yao wenyewe
Walipoulizwa na kama ni sahihi kutumia fedha za umma kugharamia matangazo ya moja kwa moja ya
vikao vya Bunge, asilimia 80 ya wananchi wamesisitiza kuwa matangazo hayo yana umuhimu sambamba
na huduma nyingine za jamii.
• Wananchi walio wengi (88%) wanasema matangazo ya vikao vya Bunge yarushwe moja kwa moja
bila kujali gharama.
• Watanzania wanaunga mkono kwa kiwango kikubwa (asimilia 75) suala la kuruhusiwa kwa
vyombo binafsi vya habari kurusha matangazo ya moja kwa moja ya viako vya Bunge iwapo serikali
imeshindwa kuyagharamaia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema: “Suala la kusitisha matangazo ya moja
kwa moja ya vikao vya Bunge la Tanzania limezua mjadala mzito miongoni mwa watanzania.
Kupitia
Sauti za Wananchi, tunaona wazi kabisa shauku kubwa ya wananchi ya kutaka kuwaona na kuwasikia
wawakilishi wao bungeni kwa macho na masikio yao wenyewe. Je, serikali iko tayari kuyapokea
matakwa ya watanzania walio wengi katika jambo hili? Ikibadilisha maamuzi yake na kurudisha
matangazo haya itakua ishara nzuri ya nia yake ya kuimarisha uhusiano wa karibu zaidi kati ya
wananchi na wabunge wao.”
Post a Comment