Loading...

BREAKING NEWS: KIGINGI KINGINE CHAPATIKANA NDANI YA MKUTANO MAALUM WA CCM

MKUTANO Maalum wa CCM ambao ni kwa ajili ya kumkabidhi uenyekiti Rais John Magufuli umeota mbawa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni ukosefu wa fedha za kuandaa mkutano huo.
 
Mkutano huo ulipangwa kufanyika mwezi huu lakini hadi kufikia jana jioni hakukuwa na dalili za kufanyika kwa mkutano huo zaidi ya kuwapo kwa taarifa kuwa chama hicho tawala kinahaha kusaka fedha kwa ajili ya kuuitisha mkoani Dodoma.
Hata hivyo, Nipashe haikuweza kuthibitisha ukweli wa madai hayo ya kuwapo kwa ukata unaokwamisha mkutano mkuu maalum baada ya jitihada za kupata kauli ya wasemaji rasmi wa CCM akiwamo Ole Sendeka kushindikana jana.
Hata hivyo, licha ya kukosekana kwa taarifa rasmi za CCM, chanzo kimoja ndani ya chama hicho kiliiambia Nipashe kuwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana ndiyo unaotajwa kukausha kwa kiasi kikubwa akaunti zote za chama hicho kutokana na gharama zilizojitokeza wakati wa mikutano ya kampeni.
Rais John Magufuli alipeperusha vyema bendera ya CCM baada ya kuibuka na ushindi wa asilimia 58.46 ya kura zote halali zilizopigwa.
Taarifa zaidi zinadai kuwa habari ya ukata huo ndani ya CCM imeelezwa pia kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka, wakati akikanusha uvumi ulioanza kuenea kuwa mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Rais mstaafu wa awa,mu ya nne Jakaya Kikwete, anang’ang’ania kubaki katika nafasi hiyo badala ya kumpisha Rais Magufuli kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake katika nafasi hiyo.
Katika kutekeleza dhana ya kofia mbili, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, aliachia madaraka mapema kabla ya kutimiza kipindi chake cha uongozi ili kumpisha Rais Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005; hivyo Kikwete anatarajiwa pia kuiacha nafasi hiyo mapema ili kumpisha Magufuli.
Katika taarifa yake ya Mei mwaka huu, Ole Sendeka alinukuliwa akisema kuwa dhamira ya kufanya Mkutano Mkuu Maalum utakaomkabidhi Magufuli uenyekiti iko pale pale, bali kilichopo sasa ni kutafuta fedha za kugharimia mkutano huo wa Juni (mwezi huu).
Ole Sendeka alisema kwenye taarifa hiyo kuwa taratibu za kutafuta fedha za kuendesha mkutano huo zinaendelea na kwamba zikikamilika ndipo tarehe itapangwa.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya CCM kinaeleza kuwa kauli ya Ole Sendeka inadhihirisha kuwa ukata utokanao na matumizi ghali wakati wa kampeni za uchaguzi umechangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maandalizi ya mkutano huo maalum na hivyo kumchelewesha Rais Magufuli kushika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho tawala.
“Kila mmoja anatamanani Rais Magufuli ashike uenyekiti ndani ya CCM haraka iwezekanavyo ili afufue mapenzi ya wananchi kwa CCM baada ya kuyumba kutokana na kuhusishwa mara kadhaa na masuala ya ufisadi….Magufuli hana msamaha na mafisadi na watu wote wanajua hilo.
Hivyo kukosekana fedha za mkutano huo maalum kwa sasa ni pigo kwa sababu kunachelewesha uenyekiti wa Rais Magufuli,” chanzo kingine ndani ya CCM kiliiambia Nipashe katikati ya wiki.
Aidha, kauli ya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa CCM, ya kutaka mkutano huo uwe na ajenda moja tu ya kukabidhi madaraka, inadhihirisha vilevile kuwa kuna ukata mkubwa wa fedha na hivyo hawatarajii mkutano huo uchukue muda mrefu na kugharimu fedha nyingi zaidi.
Kutokana na pendekezo la Mwenyekiti Kikwete, ni dhahiri kuwa mkutano huo maalum hautarajiwi kuchukua zaidi ya siku mbili ili kukamilisha ajenda hiyo moja pekee, yaani ya kumpa fursa Rais Magufuli kushika uenyekiti.
Kwa kawaida, Mkutano Mkuu hujumuisha wajumbe wasiopungua 2,400 ambao hupaswa kulipwa posho ya usafiri na malazi katika kipindi chote wawapo mkoani Dodoma.
“Hali hii ni nadra na nadhani ni mara ya kwanza kwa CCM kushindwa kupanga tarehe rasmi ya Mkutano Mkuu kutokana na ukjosefu wa fedha… inawezekana hali ni mbaya,” chanzo kilidai.
Inaelezwa kuwa chama hicho kinahitaji walau Sh. bilioni moja kwa ajili ya kufanikisha gharama za mkutano huo maalum.
Mjumbe mmoja aliyehudhuria Mkutano Mkuu wa chama hicho uliompitisha Magufuli kuwa mgombea urais wa chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana, aliiambia Nipashe kuwa walilipwa Sh 400,000 kila mmoja baada ya kuwapo Dodoma kwa siku tatu; yaani siku ya kwanza ya kuwasili na kutoa taarifa, siku ya pili kufanyika mkutano mkuu na siku ya tatu iliyokuwa ya kuondoka.
Taarifa nyingine za uhakika zinadai kuwa hadi sasa, wapo watu kadhaa waliotoa huduma mbalimbali kwa CCM katika harakati za kufanikisha ushirikin wao katika uchaguzi bado hawajamaliziwa malipo yao kutokana na ukata.
Inaelezwa kuwa baadhi ya wanaoidai CCM hadi sasa ni wasaniii mbalimbali wakiwamo wa filamu marufu kama ‘Bongo Movie’ na pia baadhi ya wanamuziki wa kizazi kipya (bongofleva) ambao walishiriki bega kwa bega katika mikutano ya kampeni ya chama hicho.
Mmoja wa wasanii hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema hadi sasa bado anadai fedha nyingi (hataji akihofia kujulikana), lakini sasa anaelekea kukata tamaa kwa sababu haoni dalili zozote za kulipwa na kwamba kila anayemuulizia miongoni mwa wale waliomfuata na kumpa ‘tenda’ hiyo amekuwa akirushia mpira kwa wengine.
OLE SENDEKA, KINANA
Jana, gazeti hili lilimtafuta Ole Sendeka ili azungumze siku ya kufanyikia kwa mkutano huo mkuu maalum lakini jitihada za mwandishi ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kutopokewa licha ya kuita mara kadhaa na pia hakukuwa na majibu hata baada ya kutumiwa ujumbe mfupi.
Wakati fulani alipopigiwa, Ole Sendeka alikata simu na mara nyingine ilipokewa lakini hakukuwa na majibu.
Alitumiwa ujumbe wa simu lakini hakutoa majibu yoyote licha ya ripoti kuonyesha kuwa ujumbe huo ulimfikia mhusika.
“Mheshimiwa Sendeka, hapa ni Nipashe tunakupigia kutaka kujua kama tarehe ya Mkutano Mkuu Maalum imeshapangwa… ni lini maana mliahidi kwamba utafanyika Juni,” ulisomeka ujumbe huo kwenda kwa Sendeka majira ya saa 3:59 asubuhi.
Majira ya saa 12: 32 mchana, Nipashe pia ilimpigia Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, ambaye naye simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.
Kinana naye alitumiwa ujumbe unaofanana na ule uliotumwa kwa Ole Sendeka, lakini naye hakujibu chochote licha ya taarifa ya mrejesho wa simu kuonyesha kwamba ujumbe huo umefika na kupokewa kupitia namba ya simu yake.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi ambaye pia ni Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni na Wasanii, Nape Nnauye, alisema kuwa yeye si msemaji wa chama kwa sasa.
“Siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu mimi si msemaji wa chama kwa sasa… watafute wasemaji wa chama tafadhali,” alisema Nape kuiambia Nipashem jana.
Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Mweka Hazina wa chama hicho Zakia Meghji majira ya saa 1: 18 mchana, lakini naye hakupokea simu yake licha ya kupigiwa kwa zaidi ya mara tatu Meghji naye alitumiwa ujumbe kama uliotumwa kwa Kinana na Sendeka lakini kujibu chochote licha ya ripoti kuonyesha kuwa umemfikia.
Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula alipotafutwa majira ya 2:15 mchana simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa ambapo naye hakujibu ujumbe aliotumiwa kuhusu suala hilo licha ujumbe kuonyesha umemfikia.
Mei 4 mwaka huu, lilijitokeza kundi linalodaiwa kumshinikiza Mwenyekiti wa sasa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete asimkabidhi uenyekiti Rais Magufuli kabla ya muda wake kumalizika.
Ilielezwa mwezi Mei kuwa kundi hilo limejipenyeza hadi vikao vya juu kama Kamati Kuu vikimshinikiza Mwenyekiti Kikwete aendelee hadi Oktoba mwakani muda wake utakapokwisha.
Ilielezwa kuwa mpango huo wa kutaka Kikwete aendelee na wadhifa huo ni mahsusi kwa ajili ya kudhibiti kasi ya Magufuli kutokana na hofu ya mtandao uliopo kuona kwamba dawa pekee ya kutekeleza azimio lao hilo ni Kikwete kubaki na uongozi wa chama.
Chanzo kimoja kilisema kuwa kuna hofu imejengeka ndani ya mtandao wa sasa wa CCM kwamba akikabidhiwa madaraka ya chama, Rais Magufuli atawatimua kama anavyofanya serikalini.
Baada ya taarifa za Kikwete kutaka kung’ang’ania madaraka kuzagaa, CCM haraka haraka kupitia msemaji wake Ole Sendeka ilikanusha njama za Mwenyekiti huyo kutaka kung’ang’ania madaraka na kuahidi kuwa mpango wa kumkabidhi Magufuli chama mwezi Juni uko palepale.
Ingawa mwezi Juni unaelekea katikati hakuna dalili za kufanyika kwa mkutano huo na viongozi wote wa juu wa chama hicho wameamua kutozungumzia suala hilo.
Akiwa mkoani Singida kwenye sherehe za miaka 39 ya CCM, Kikwete alikaririwa akisema kuwa sherehe hizo ndizo za mwisho kwake, kauli inayomaanisha kuwa atamwachia nafasi hiyo Rais Magufuli mapema, kama walivyofanya watangulizi wake, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top