Nikatoa maelezo nikiwatetea vijana hao nikasema kwamba utaratibu wa kwenda Chuo kikuu bila kupita A-Level ni utaratibu rasmi unaotambulika nchini. Na wapo wengi waliotumia utaratibu huo na wakafika mbali. Katika kutoa mfano wa mmoja wa watu waliotumia utatatibu huo nikamtaja Profesa Mark Mwandosya, kwamba yeye baada ya kumaliza kidato cha nne alijiunga na chuo cha ufundi (DIT) kisha akadahiliwa chuo kikuu.
Jana nikapata taatifa kuwa Profesa Mwandosya amenijibu. Nikatumiwa taarifa ya majibu yake. Sikutaka kuamini taarifa hiyo kwa haraka hadi ndugu Gabriel Mwang'onda alipowasiliana nami na kunihakikishia kuwa ni majibu halisi kutoka kwa Profesa Mwandosya mwenyewe.
Kwanza nimpongeze Profesa Mwandosya kwa kuona umuhimu wa kunijibu. Ni viongozi wachache sana wanaotambua nguvu ya mitandao ya kijamii. Kwahiyo kama hoja yangu ilimfikia kupitia mitandao na akaweza kisoma na kujibu ni jambo la kupongezwa.
Lakini maelezo ya Mwandosya hayajajibu hoja ya msingi badala yake ametoa ufafanuzi juu ya elimu yake. Ingekuwa mahakamani Mwandosya angekua amejadili suala ambalo sio sehemu ya mjadala (matter which is not in dispute).
#MAELEZO_YA_MWANDOSYA
Mwandosya anakiri kwamba ni kweli alisoma chuo cha Ufundi Dar (DIT) lakini anasema kuwa si kweli kwamba hakusoma A-Level. Anasema akiwa DIT alisoma ufundi wakati huohuo akisoma masomo ya form five na six.
Anasema serikali kwa wakati huo ilianzisha mpango maalumu wa kuchukua wanafunzi wenye ufaulu wa juu ktk masomo ya sayansi na kuwasajili katika tasisi mbili ambazo ni sekondari ya Kibaha na Chuo cha Ufundi Dar (DIT) kwa masomo ya sayansi.
Mpango huo ulidumu kwa miaka mitatu kati ya mwaka 1968 na mwaka 1971. Kwa mujibu wa Mwandosya katika "mpango huo maalumu" wanafunzi walisoma masomo ya ufundi (FTC) wakati huohuo wakisoma masomo ya A-level. Hii ilimuwezesha yeye kudahiliwa chuo kikuu cha Aston nchini Uingereza kwa kuwa alikuwa amehitimu pia kidato cha sita nje ya masomo ya ufundi aliyokua akisomea.
Profesa Mwandosya ametaja baadhi ya maprofesa wenzake waliopita kwenye utaratibu huo maalumu ambao ni pamoja na Prof.Mugurusi, na Prof.Mathew Luhanga etc.
#HOJA_YA_MSINGI
Hoja ya msingi haikua Elimu yaProfesa Mwandosya. Hoja ya msingi ilikua utaratibu wa kwenda chuo kikuu bila kupita A-Level. Mwandosya alitumika tu kama mfano, kama ambavyo ningeweza kutumia mfano wa mtu mwingine.
Kwahiyo nilitegemea Mwandosya ajibu kwamba utaratibu huo UPO ila mfano uliotumika kwake si sahihi, au akanushe kwamba utaratibu huo HAUPO. Yani aseme hakujawahi kuwa na utaratibu wa kwenda chuo kikuu kwa kutokea FTC bila kupita A-Level, kwa hiyo maelezo ya Malisa ni ya uongo. Lakini Mwandosya hajafanya hivyo.
Alichofanya ni kutoa ufafanuzi juu ya elimu yake kana kwamba tulikua tuna hofu na elimu yake. Hakuna mtu mwenye hofu na elimu ya Profesa Mwandosya, tunajua yeye ni msomi mzuri anayetambulika kimataifa.
Ambacho alitakiwa kueleza ni kujibu hoja ya msingi then akanushe mfano uliomhusu yeye. Kwa mfano angeweza kusema "utaratibu wa kwenda chuo kikuu bila kupita A-level ni utaratibu rasmi unaotambulika ila mimi sikutumia utaratibu huo" kisha ndo akaeleza yeye alitumia utatatibu gani.
Lakini andiko lake kuwa alidahiliwa chuo kikuu kwa matokeo yake ya form six na sio cheti cha FTC ni kama vile anasema huwezi kwenda chuo kikuu ukitokea chuo cha ufundi (FTC) au vyuo vingine vya kawaida jambo ambalo si kweli. Yawezekana Mwandosya hakukusudia kumaanisha hivi lakini ndivyo watu walivyomuelewa.
Hoja ya msingi ni je, hivi haiwezekani kwenda chuo kikuu bila kupita A-level? Kama Mwandosya anasema yeye alipita A-level, je hakuna wengine waliofika chuo kikuu bila kupita A-level??
Ktk maelezo yake Mwandosya anasema utaratibu wa kusoma elimu ya ufundi (FTC) na masomo ya A-level kwa pamoja ulikua ni "mpango maalumu" uliodumu kwa miaka mitatu tu (1968 hadi 1971).
Maana yake ni kwamba kabla ya mwaka 1968 wanafunzi wa DIT walikua wakisoma FTC tu bila kuchanganya na A-level, na baada ya mwaka 1971 wanafunzi waliendelea kusoma FTC tu bila masomo ya ziada ya A-Level. Kwahiyo waliofanikiwa kusoma "two in one" yani FTC na wakati huohuo wakisoma A-Level ni akina Mwandosya tu (1968 - 1971).
Sasa je Mwandosya anataka kutuambia kuwa wale waliomaliza FTC kabla yao, au baada yao je, hawakupata nafasi za kwenda vyuo vikuu kwa sababu hawakuwa na masomo ya A-level?? Jibu si kweli.
Mimi binafsi nawafahamu wasomi wengi tu wazuri waliosoma FTC na walipomaliza wakadahiliwa vyuo vikuu bila kusoma A-Level kama Mwandosya. Na utaratibu huu umekua ukitumika kwa muda mrefu hadi serikali ilipobadilisha mtaala wa FTC kuwa Ordinary Diploma.
Na hadi sasa hivi wahitimu wa kidato cha 4 waliofanya vizuri masomo ya sayansi wanadahiliwa kusoma Ordinary Diploma kwenye vyuo vya ufundi kisha wanajiunga na vyuo vikuu kusomea shahada mbalimbambali za Uhandisi bila kupita A-Level.
Kwahiyo nihitimishe kwa kusema kwamba maelezo ya Profesa Mwandosya ni mazuri lakini ametoka nje ya hoja. Kama yeye alisoma FTC na A-Level kwa pamoja, haimaanishi kuwa hakuna waliosoma FTC peke yake na wakaenda vyuo vikuu. Wapo waliosoma FTC na walipohitimu wakaenda vyuo vikuu bila kufanya masomo ya ziada ya A-Level kama yeye.
Hivyo basi kwa kuwa inawezekana kwenda chuo kikuu bila kupita A-Level, hatuwezi kuwahukumu wanafumzi wa UDOM waliotoka kidato cha 4 kwenda kusomea Diploma maalumu ya ualimu wa sayansi kwa miaka mitatu. Utaratibu waliotumia upo sahihi kabisa na wakimaliza wanaweza kujiunga na vyuo vikuu wakasomea Shahada (degree) bila tatizo lolote.
Mnaweza kumfikishia salamu hizi baba yangu Profesa Mwandosya as matter for noting.
Asanteni,
Malisa G.J
Post a Comment