BUNGE la Tanzania limeahirishwa. Ni kutokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kugomewa kuwasilisha hoja binafsi kuhusu wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kusimamishwa, anaandika Faki Sosi.
Hatua hiyo imetokana na Tulia Ackson, Naibu Spika kugomea mwongozo uliotolewa na mbunge kutoka Ukawa kuhusu kujadiliwa taarifa ya kusimamishwa kwa wanafunzo kutoka chuo hiko.Taarifa kutoka bungeni zinaeleza kwamba, Ackson aligomea taarifa hiyo jambo limezua mzozo na hatimaye wabunge kuamua kutoka nje ikiwa ni ishara ya kutoridhika na uamuzi wa kiti cha spika. Mwanahalisi Online linaendelea kufuatilia.
Juzi Udom kilitoa taarifa ya kusimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya ualimu wa Sayansi, Hisabati na Teknolojia kwa ngazi ya Stashahada na kisha kutaka waondoke chuoni hapo mara moja.
Tangazo hilo liliwataka wanafunzi hao kuondoka kati ya juzi na jana saa 12 jioni. Tangazo hilo lilieleza kuwa kutokana na matatizo yaliyopo katika ufundishaji wa stashahada hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imeamua wanafunzi hao kurejea majumbani na kwamba wataelezwa mustakabali wao “mapema iwezekanavyo”.
Kozi ya Stashahada ya Ualimu wa Sayansi, ilianzishwa maalumu kwa agizo la Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kwa lengo la kuziba pengo la walimu wa sayansi na ilikuwa inatolewa UDOM pekee.
Waliokuwa na sifa za kujiunga na kupewa mikopo ni wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo ya sayansi.
Wanafunzi hao waliokuwa wamekopeshwa na serikali wamesimamishwa siku mbili baada ya wenzao zaidi ya 480 wa Chuo Kikuu cha St. Joseph kusimamishwa baada ya kubainika kutokuwa na sifa za kudahiliwa.
Post a Comment