Loading...

HII NDIO SHULE YA MSINGI ILIYOKO DAR ES SALAAM ILIYOVUNJA REKODI DUNIANI KWA TUKIO LA AINA YAKE


Shule ya Msingi Majimatitu ya Temeke jijini Dar es Salaam, imeingia kwenye rekodi ya aina yake hapa nchini na pengine Afrika kutokana na kusajili wanafunzi 1,022 wa darasa la kwanza, idadi ambayo inatosha kuanzisha shule nyingine.
Idadi hiyo imeifanya Majimatitu kuwa na jumla ya wanafunzi 6,000.
 
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa shule hiyo ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosomea chini ya miti, lakini ikiwa na wastani mzuri wa ufaulu wa darasa la saba wilayani Temeke kwa shule za serikali.
 
Shule hiyo ina madarasa 22 na ili iweze kumudu idadi hiyo ya wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka la saba inahitaji nyongeza ya madarasa 109. Aidha inatakiwa kuwa na matundu 239 ya choo lakini kwa sasa yako matundu 36 tu.
 
Gazeti hili lilifanya mahojiano na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Abdul Ngomi, ili kujua kwa nini wazazi wengi wanapendelea watoto wao wasome shule hiyo ili hali maeneo ya jirani kuna shule nyingi nyingine.
 
MAZINGIRA, UFAULU
Mwalimu Mkuu huyo alisema shule hiyo ina mazingira mazuri na imekuwa ikifaulisha kwa kiwango kizuri kila mwaka hivyo wazazi wengi hawataki watoto wao wajiunge na shule nyingine zaidi ya hiyo.
 
Akitoa takwimu za ufaulu, Mwalimu Mgomi alisema tangu mwaka 2007, shule yake imekuwa ikipata ufaulu mzuri, ikiwemo asilimia 97 waliyopata mwaka jana jambo linalowavutia wazazi.
 
Alisema mwaka 2014 walitoa wanafunzi 25 waliokwenda katika shule za sekondari za ufaulu wa juu na watatu waliochaguliwa katika shule za vipaji maalum.
 
“Pamoja na kuwa na wanafunzi wengi, walimu wangu wamejipanga vizuri kuhakikisha ubora na kiwango cha utoaji elimu unabaki palepale, jambo ambalo wengi wanashindwa,” alisema.
 
Alisema kitu kingine kinachovutia wazazi wengi ni shule hiyo kushika nafasi ya kwanza kwenye mashindano mbalimbali na kuifanya ofisi ya Mwalimu Mkuu kuwa na tuzo nyingi.
 
Alisema kwa miaka saba mfululizo Shule ya Msingi Majimatitu imeshika nafasi ya kwanza katika uhifadhi wa mazingira kwa Mkoa wa Dar es Salaam na shule bora inayozingatia weledi katika ufundishaji.
 
Wanafunzi wa madarasa mawili ya saba na sita walikutwa wakifundishwa wakiwa wamekaa chini ya mti kwa kutenganishwa na ubao maalum uliojengwa kwa matofali.
 
Wanafunzi hao walionekana kupata shida ya usikivu kutokana na sauti za walimu wanaowafundisha na zile za wanafunzi kuingiliana.
 
Hata hivyo, mwalimu mmoja aliyekutwa akifundisha somo la sayansi kwa darasa la sita, alisema  wamebuni njia hiyo ili kuhakikisha wanafunzi hao wanaendelea kupata elimu katika mazingira hayo hayo magumu.
 
Maeneo yote yaliyokuwa wazi katika shule hiyo sasa yamegeuzwa kuwa madarasa na walimu wameonekana kutojali sana hali hiyo na wanaonekana wakiendelea kuchapa kazi kama kawaida.
 
Baadhi ya maeneo yaliyogeuzwa kuwa madarasa ni kuta za nje ya shule, jiko la kupikia chakula kwa wanafunzi, chini ya miti na mahema mawili yaliyowekwa mbele ya ofisi ya mwalimu mkuu.
 
Kutokana na ubunifu wa walimu kwa kushirikiana na Manispaa, kumetengenezwa mbao maalum ya kufundishia kila mahali kwa ajili ya kutumiwa na walimu na wanafunzi.
 
“Hakuna njia sahihi ya kukabiliana na changamoto ya madarasa kama hii tuliyoibuni, tunawafundisha kwa kutumia ubao huu, madarasa yote mawili yanaweza kusoma kwa wakati mmoja bila matatizo,” alisema mwalimu huyo ambaye alikataa kutaja jina lake.
 
Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mgomi, alisema wameamua kutumia mbinu hiyo ya ufundishaji darasa pacha kwa lengo kuwafikia wanafunzi wote kwa wakati mmoja na kwamba hilo lilifanyika ili kuwapa nafasi wanafunzi wa darasa la kwanza kutumia vyumba hivyo.
 
“Idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza wameenea madarasa yote ya shule yetu, hivyo tunatumia ubunifu kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa masomo wakati suala hili linaendelea kufanyiwa kazi,” alisema Mwalimu Mgomi.
 
Kutokana na changamoto hiyo, mwalimu mmoja amekuwa akijikuta akifundisha wanafunzi 180 kwa wakati mmoja, idadi ambayo ni sawa na mikondo minne yenye idadi ya watoto 45 kila darasa.
 
Shule hiyo pia inakabiliwa na tatizo la maji safi na salama, kutokana na kisima kilichopo kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 8000, badala ya 32,000 zinazotakiwa ili kutosholeza mahitaji ya kiwango hicho cha wanafunzi. 
 
WAZAZI WASEMA WATABANANA HAPAHAPA MAJIMATITU
Baadhi ya wazazi waliozungumza na Nipashe walisema pamoja na serikali kuingilia kati kwa kuboresha shule nyingine ili kuwashawishi kuwapeleka watoto wao huko, lakini wataendelea kuandikisha watoto wao kwenye shule hiyo kutokana na ubora wa elimu.
 
Wakizungumza mara baada ya kusikiliza hotuba iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa Mecky Sadick kwa wazazi hao, walisema wananchoangalia ni ubora wa elimu, mazingira na usalama wa watoto wao.
 
Salima Juma alisema watoto wake watatu walisoma katika shule hiyo na wamefaulu vizuri huku akisifia namna walimu wa shule hiyo wanavyojituma kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri.
 
“Hata kama wakijenga shule nyingine au kujenga madarasa, bado kwa upande wangu nitawandikisha watoto wangu katika shule hii siendi popote,” alisema Salima.
 
Mzazi mwingine Abillah Shimweta, alisema tofauti na shule nyingine za serikali, walimu wa shule hiyo wamekuwa walezi na wafuatiliaji kiasi ambacho mzazi anashirikishwa kwa kila kitu kuhusu mtoto wake.
 
Alisema, imefikia wakati walimu wanakaa na mzazi kujadili maendeleo ya mtoto pamoja na kumpatia ushauri kuhusu hatua za kuchukua iwapo mtoto anaonekana anarudi nyuma kimasomo.
 
“Mwaka uliopita mtoto wangu alirudi nyuma kidogo, niliitwa hapa tulikaa pamoja na kujadiliana ili kwa pamoja tuchukue hatua, suala kama hili kwa shule nyingine hakuna,” alisema Shemweta.
 
"Tunawapongeza walimu kwa kweli."
 
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mianzini, Saidi Mpeta, alisema yeye na kamati yake ya mtaa walijitahidi kuwahimiza watu kutumia shule nyingine baada ya kuona shule ya Majimatitu imeelemewa, lakini ilishindikana.
 
“Mimi na kamati yangu tuliamua kupita kila nyumba kuwaomba waende kuandikisha watoto katika shule zingine za jirani lakini hakuna aliyetusikia na kila mmoja aling’ang’ania mtoto wake asome hapa,” alisema Mpeta.
 
MSAADA WA DHARULA
Mpeta alisema kunahitajika nguvu za ziada kwa ajili ya kuongeza vyumba ili wanafunzi waweze kusoma vizuri hasa katika kipindi hiki cha mvua.
 
Aliziomba taasisi zisizo za kiserikali, kampuni na watu binafsi kusaidia angalau kwa kujenga madarasa kwa lengo la kuwaokoa watoto hao.
 
“Changamoto hii ni kubwa, serikali pekee yake haiwezi kupata ufumbuzi kwa muda unaotakiwa, tunaomba watu wengine wajitokeze kusaidia watoto hawa waondokane na tatizo la kusoma nje,” aliongeza.
 
SERIKALI YAINGILIA KATI
Juzi, Mkuu wa Mkoa Sadick akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, walifanya ziara shuleni hapo na kuahidia kujenga madarasa 10 ya dharula wakati mikakati mingine kuongeza vyumba ikifanyiwa kazi.
 
Mkuu wa Mkoa alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, wanatarajia kujenga jengo la orofa tatu jirani na shule hiyo ambalo itakuwa na vyumba 30 vya madarasa.
 
“Nia ya serikali ni kumaliza tatizo hili la Majimatitu na kwa kuanzia tutajenga madarasa 10, tutaongeza madarasa matano katika kila shule moja zilizo jirani ili wazazi waende kuandikisha watoto huko,” alisema Sadick.
 
Alitaja shule hizo kuwa ni Mianzini, Machinjioni, Mbande, Chamazi na kujenga shule mpya ya Majimatutu B.
 
Katika mpango huo, Serikali imetwaa eneo lilokuwa likimilikiwa na Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) kwa lengo la kujenga shule nyingine ambayo itasaidia shule hiyo kupumua.
 
“Serikali imekubaliana na UWT kuchukua eneo lao kwa nia ya kujenga shule mpya pale, tukifanikiwa hilo Majimatitu itapumua,” alisema zaidi Mkuu wa Mkoa.
 
MWANZO WA MAJIMATITU
Shule ya Mjimatitu imechukua jina la eneo hilo, lenye maana ya ‘Maji meusi’ kwa lugha ya kabila la Wazaramo.
 
Shule hiyo ilianza kujengwa mwaka 2001 ikiwa na darasa moja kwa ushirikiano wa wananchi wa eneo hilo na Shirika moja la kidini la Holy Union chini ya uongozi wa Mtawa, Aneth Farell.
 
Mwaka 2002 shule hiyo ilianza ikiwa na wanafunzi 220, kati ya hao 100 wa darasa la pili walihamishiwa hapo wakitokea shule ya Nzasa na walimu wanane pekee.
 
Kwa sasa shule hiyo yenye wanafunzi 6,000 ina walimu 77, wanaume wakiwa 12 na wanawake 65.
 
ILIVYOIBULIWA
Wiki iliyopita Nipashe ilitoa taarifa za mwenendo wa uandikishaji kwenye shule hiyo na kumnukuu Afisa Elimu wa Temeke, Honorina Mumba, ambaye alisema imeongoza kwa kuandikisha wanafunzi 1,000, jambo ambalo halijawai kutokea.
 
Shule nyingine zilizofuatia kwa kuandikisha watoto wengi ni Kiramba (502), Kiburugwa (600), Mbande (873), Amani (587)Chamazi (722), Buza (632) na Kiburugwa (781).
CHANZO: NIPASHE    

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top