Loading...

Serikali yatadhaharisha kimeta

 Serikali imetoa tahadhari ya mlipuko wa kimeta, moja ya magonjwa yanayoenezwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, katika mkoa wa Kilimanjaro.
 
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
 
Wizara ilisema siku za karibuni ugonjwa wa Kimeta ulitokea mkoani Kilimanjaro ambapo wagonjwa 23 waliugua na kuripotiwa katika kijiji cha Rauya, kata ya Marangu Mashariki, Wilaya ya Moshi Vijijini.
 
Taarifa ilisema ugonjwa huo ulianza kwa mgonjwa mmoja aliyeugua baada ya kuchinja ng'ombe na mbuzi waliokuwa wamekufa ambaye; alitibiwa katika hospitali ya KCMC na kupona.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na timu ya Mkoa na Wilaya ilifanya uchunguzi.
 
Katika uchunguzi huo, imeelezwa, ilibainika kuwa watu 23 waliugua na walihusika moja kwa moja katika uchinjaji au upishi wa nyama za ng'ombe wagonjwa au waliokufa waligundulika kuwa na dalili za ugonjwa wa Kimeta.
 
Taarifa ilisema timu ya wataalamu wa afya kutoka ngazi ya Taifa ilikwenda kushirikiana na timu ya Mkoa na Wilaya husika katika uchunguzi na udhibiti wa ugonjwa.
 
“Ufuatiliaji wa waliokula nyama ya ng'ombe waliougua au kufa ulifanyika ambapo wote wamepata dawa za kinga, jumla ya watu 904 walihusishwa na kula nyama za ng'ombe waliokwishakufa ambapo Wilaya ya Siha ni 836 na Wilaya ya Moshi Vijijini walikuwa 68,” ilisema taarifa ya Wizara. 
 
"Ugonjwa wa Kimeta unasababishwa na aina ya bakteria aitwaye Bacillus anthracis ambaye anashambulia wanyama mwitu, wafugwao pamoja na binadamu."
 
Taarifa ilifafanuwa kuwa ugonjwa huo unaambukizwa kutoka mnyama kwenda kwa binadamu au kutoka binadamu mmoja kwenda mwingine au kwa njia ya kugusa nyama, damu na majimaji kutoka kwa mnyama au mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo kutokana na kula nyama ya mnyama aliye mgonjwa.
 
“Wizara inatoa rai kwa jamii kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu ambazo ni pamoja na kuepuka kula nyama inayotokana na mnyama aliye mgonjwa au aliyekufa," ilisema taarifa hiyo na kusisitiza wananchi wanapaswa kutumia nyama iliyothibitishwa na mtaalamu wa mifugo.”
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

CodeNirvana
Newer Posts Older Posts
© Copyright KAZI YANGU | Designed By AFROPIXELS MEDIA CO. LTD
Back To Top